Chuo cha Elimu
na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha VETA Dakawa kimeanza kutoa mafunzo ya ufugaji
bora wa kisasa wa nyuki.
Mkuu wa chuo
cha VETA Dakawa Beatus Nyakunga amesema kuwa mafunzo hayo yameanza kutolewa kwa
muda mfupi ambapo kijana anaweza kujiunga na kupata utaalam wa kutengeneza
mizinga na kufuga nyuki kisasa kwa muda wa wiki mbili.
Kwa mujibu wa
Bw. Nyakunga, mafunzo wanayoyatoa ni ya ufugaji bora na wa kisasa wa nyuki na
kwamba mizinga ya nyuki huwekwa kwenye mabanda badala ya kutundika kwenye miti.
Amesema chuo
chake kimeamua kuanzisha mafunzo hayo kutokana na ukweli kuwa mazao
yanayotokana na nyuki yanaendelea kupanda thamani kila siku na kwamba ni fursa
nzuri sana kwa vijana kujiajiri.
“Tunaamini
kuwa mafunzo haya yatasaidia vijana wengi kujiajiri wenyewe kwa sababu mazao ya
nyuki yana faida sana…Mzinga mmoja unaweza kutoa kiasi cha chini cha kilo 10 na
kilo moja ni shilingi 10,000 hadi 15,000”Alisema.
Anasema tayari
wameshavuna kilo 72 kutoka kwenye mizinga nane mwaka huu na kwamba mizinga
mingine 53 ina nyuki wanaoendelea kuchakata na kwamba wanatarajia kuvuna
mwishoni mwa mwezi huu (Aprili, 2018) na mavuno mengine ni mwezi Julai.
Bw. Nyakunga
anawahamasisha vijana na jamii kwa ujumla kuhamasika na mafunzo hayo na kuweza
kujiunga nayo kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato huku akibainisha kuwa ni
vijana 15 tu ambao wameshasomea mafunzo hayo kwa mwaka huu.
Naye mtaalamu
wa ufugaji nyuki chuoni hapo Bw. Yohana Mkonongo anasema ufugaji wa nyuki kwa
kukusanya mizinga kwenye banda una faida zaidi na uhakika wa mavuno tofauti na
ule wa kutundika mizinga kwenye miti ambapo mizinga mingi huharibiwa na wanyama
pamoja na wadudu, hunyeshewa na mvua na wakati mwingine kuungua moto.
No comments:
Post a Comment