Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeshauriwa kutumia utaratibu wa ajira za uhamisho kama moja ya njia za kupunguza changamoto ya uhaba wa watumishi unaoikabili.
Ushauri
huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael, wakati akizindua Baraza Kuu na
Wafanyakazi wa VETA, katika ofisi za VETA Makao Makuu, jijini Dar es Salaam,
siku ya Alhamisi, tarehe 26 Novemba 2020.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema utaratibu mwingine ni ule wa “Ajira Mbadala” ambao hutumika kujaza nafasi za wafanyakazi waliotoka katika utumishi wa umma kwenye taasisi hiyo. Watumishi hao ni wale waliostaafu, kuhama, kuacha au kuachishwa kazi au kufariki dunia. Alisema kwamba utaratibu huu hauna mlolongo mrefu wa uidhinishaji kwa kuwa ikama katika nafasi husika zilikuwa zimeshaidhinishwa.
“Lakini pia niseme kwamba nimeichukua changamoto yenu ya uhaba wa watumishi na naahidi kuwasaidia kupata watumishi ili kupunguza nakisi ili utendaji wa Mamlaka uboreke na muweze kutayarisha mafubndi stadi mahiri na wa kutosha. Leteni, njooni tuzungumze, nina imani hatutashindwa,” alisema.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu alisema kuwa moja ya changamoto kubwa ambazo VETA inakabiliwa nazo ni uhaba wa watumishi, hasa kada ya ualimu, hali inayochangia watumishi waliopo kubeba mzigo mzito wa majukumu.
Alisema
VETA ina upungufu wa watumishi 562 ambapo kati yao 396 ni walimu wa mafunzo ya
ufundi stadi na 166 wa kada zingine.
“Kutokana na uhaba mkubwa wa watumishi, wale tuliopo tunabeba majukumu ambayo yangefanywa na watumishi wawili au watatu. Matokeo yake karibu kila siku tunafanya kazi mpaka usiku, wakati mwingine mpaka usiku wa manane, ili kuhakikisha majukumu ya Mamlaka yanakamilika. Tunabeba mzigo mzito na tunachoka sana,” Dkt. Bujulu alisema.
Alimuomba Naibu Katibu Mkuu na ofisi yake kwa ujumla kulitazama kwa jicho la karibu tatizo la uhaba wa watumishi ndani ya VETA na kulitafutia ufumbuzi, hasa kwa kuzingatia umuhimu wa majukumu ya Mamlaka hiyo katika uchumi wa Taifa, hususan ujenzi na uendeshaji wa viwanda nchini.
Bi. Neema Mwakalukwa, ambaye ni Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kusini Mashariki na Mjumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi, aliiomba Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kuangalia uwezekano wa kuiruhusu VETA kuajiri wafanyakazi wa mkataba watakaosaidia kufundisha kozi za muda mfupi na kufanya kazi zingine za uzalishaji mali, kisha kulipwa kwa vyanzo vya ndani ya Mamlaka.
“Tunaingia makubaliano ya kuwalipa watu kama vibarua. Kwa hiyo hata ikitokea anakwambia kesho au keshokutwa hataweza kuja, huwezi kumzuia kwa sababu huna mkataba naye. Unajikuta umekwama. Lakini ukiwa na mkataba naye hata kama ni wa miezi sita au mwaka mmoja unakuwa na uhakika wa uwepo wake,” alisema.
Baraza
Kuu la Wafanyakazi wa VETA lilifanya kikao chake Alhamisi, tarehe 26 Novemba
hadi Ijumaa, tarehe 27 Novemba, 2020 na kujadili mambo mbalimbali, ikiwemo
utekelezaji wa mipango ya Mamlaka kwa mwaka 2019/2020 na mipango ya Mamlaka ya
mwaka 2020/2021. Taarifa hizo zilifuatiwa na mijadala ya kina, iliyohitimishwa
kwa kuweka Maazimio ya kutekelezwa kwa mwaka 2020/2021.
No comments:
Post a Comment