Wadau wa
Sekta za Kilimo na Mifugo wameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi (VETA) kwa kuandaa mitaala yenye mchanganuo mzuri wa stadi muhimu kwa
ajili ya utoaji mafunzo ya ufundi stadi kwenye sekta hizo.
Tarehe 21
Oktoba 2021, VETA kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa Care iliratibu kikao
cha wadau wa Sekta za Kilimo na Mifugo kwa ajili ya kupitia na kutoa maoni yao
kwenye miswada ya Mitaala na Mafunzo ya Ufundi Stadi katika fani za Kilimo cha
Mazao ya Shamba (Field Crop Production) na Mazao ya Bustani (Horticultural Crop
Production) na uhuishaji wa Mtaala wa fani ya Ufugaji wa Wanyama (Animal
Husbandry).
Wadau hao
waliokutana na kupitia miswada hiyo katika hoteli ya Flomi, mjini Morogoro
walitoa pongezi nyingi kwa VETA kwa hatua hiyo wakieleza kuwa sekta hizo ni
tegemeo kubwa kwa maisha ya Watanzania wengi na kwamba iwapo mitaala hiyo
itatekelezwa ipasavyo, itasaidia vijana wengi kupata ujuzi utakaowawezesha
kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo.
Fabian Mwakatuma, Mwenyekiti Baraza la Ujuzi la Kilimo, kutoka Mfuko wa Sekta Binafsi (TPSF) alisema kuna uhaba mkubwa wa watu wenye stadi katika maeneo ya kilimo na ufugaji huku kukiwa na fursa nyingi.
Aliongeza kuwa mbali na ukweli kuwa zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo katika kuendesha maisha yao, kuna fursa nyingi za kunufaika na usindikaji wa mazao mbalimbali ya kilimo na mifugo iwapo watu watapata stadi katika maeneo hayo.
Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Stella Ndimubenya amesema VETA sasa inaweka mipango na kufanya jitihada mbalimbali zinazolenga kupanua utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi katika sekta za Kilimo na Mifugo kwa kutambua umuhimu wake katika jamii na uhitaji wa stadi kwenye sekta hizo.
Baada ya kukamilisha mitaala hii na kupitishwa na Bodi, tutaanza ku-package (kuandaa) kozi mbalimbali zinazohusiana na kilimo na mifugo kulingana na mahitaji.
Naye Meneja
Mradi wa Tajirika na Kilimo, kutoka shirika la Care alisema, wakati wa
utekelezaji mradi huo kwa kushirikiana na VETA walibaini uhitaji mkubwa wa
mafunzo ya ufundi stadi katika jamii za wakulima.
No comments:
Post a Comment