CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Wednesday 17 August 2022

VETA yajenga vyuo 25 kwa kutumia nguvukazi ya ndani

      §  Yaokoa bilioni 90

§  Kunufaisha vijana zaidi ya 18,000

§  Yatengeneza samani kupitia karakana zake


“Sio tu kuvuta watu ndani waje kuwekeza,wanaowekeza wanataka watu wanaojua nini wanafanya. Tunajenga veta kila wilaya….. tuko katika process.            Na VETA sio zile za kizamani,…..hapana. Tunajenga za kisasa zitakazowapa ujuzi. akitoka mtoto VETA ni fundi ambaye anaweza akaajirika,” Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Rais Samia alitoa kauli hiyo tarehe 4 Mei 2022, katika mahojiano ya ana kwa ana na Tido Mhando, Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Media, akifafanua juu ya namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyoandaa Watanzania kiujuzi sambamba na mikakati ya ujenzi wa uchumi wa nchi.

Miongoni mwa miradi mikubwa iliyotekelezwa na Serikali katika eneo la upanuzi wa fursa za mafunzo kwa wananchi ni ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika maeneo mbalimbali. Mwaka wa fedha 2019/2020 ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi ulipewa msukumo mkubwa zaidi ambapo Serikali ilitenga Shilingi bilioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo 25 vya ufundi stadi vya wilaya, lengo likiwa ni kupanua fursa za mafunzo hayo, kuyasogeza karibu zaidi na wananchi na kuongeza kasi ya uzalishaji nguvukazi yenye ujuzi nchini. 

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ilikabidhiwa kujenga vyuo hivyo kwa kutumia nguvukazi ya ndani, yaani Force Account.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore anazitaja wilaya zilizohusika katika mradi huo kuwa ni Pangani, Mkinga, Korogwe, Kilindi, Uyui, Igunga, Ikungi, Kishapu, Rufiji, Mafia, Ukerewe, Kwimba, Masasi, Ulanga, Mbarali, Chunya, Butiama, Uvinza, Iringa Vijijini, Buhigwe, Chemba, Bahi, Monduli, Longido na Lushoto. Vyuo hivyo vitakapoanza kutoa mafunzo, vijana wapatao 18,500 wanatarajiwa kunufaika na ujuzi utakaotolewa katika vyuo hivyo kwa kila mwaka.

 “Fedha ya ujenzi iliyotolewa na Serikali katika awamu ya kwanza iliwezesha utekelezaji wa mradi kwenye vyuo vyote 25 kufikia wastani wa asilimia 79. Ili kukamilisha ujenzi huo, Serikali ilitoa tena jumla ya Shilingi bilioni 28.7 kutoka kwenye fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 20zilikuwa kwa ajili ya umaliziaji wa ujenzi (Vifaa na Ufundi) na Shilingi bilioni 8.7 ni kwa ajili ya utengenezaji wa Samani za vyuo vyote 25,” anafafanua CPA Kasore.  

Katika mradi huo, VETA pia ilipewa jukumu la kutengeneza samani, kazi ambayo imefanywa kupitia kiwanda chake cha Samani kilichopo jijini Dodoma na katika Karakana za vyuo vya VETA vya Dar es Salaam, Kihonda, Mikumi, Mbeya, Lindi, Mwanza, Shinyanga, Tabora na Kigoma. Jumla ya samani mbalimbali 39,750 zinatengenezwa kwa ajili ya vyuo 25 vya Wilaya zikihusisha za maofisini, madarasani, karakana, mabweni ya wanafunzi, bwalo la chakula, kumbi za mikutano na nyinginezo. 

Ujenzi wa vyuo hivyo kwa kutumia Force Account, umekuwa na manufaa mengi, miongoni mwake ni kupunguza gharama za ujenzi.

Mwenyekiti wa Bodi ya VETA, Ndugu Peter Maduki anafafanua,awali tulikuwa tukitumia wastani wa shilingi bilioni 6 katika ujenzi wa chuo kimoja cha wilaya  kwa kutumia wakandarasi. Lakini sasa tumetumia wastani wa shilingi bilioni 2.4 kwa chuo kimoja. Kwa kuzingatia wastani huo Mamlaka imeokoa takribani shilingi bilioni 3.6 kwa kila chuo na kwa vyuo 25 vyote ni shilingi bilioni 90.”

Mradi pia umetoa fursa ya kuimarisha stadi za ujuzi kwa wanafunzi na wahitimu wa ufundi stadi walioshiriki mafunzo kwa vitendo kwenye maeneo mbalimbali ya mradi.

Halima Amani Kalunga, fani ya Uundaji na Uungaji Vyuma, chuo cha VETA Tabora ni miongoni mwa wanafunzi walioshiriki kikamilifu katika utengenezaji wa samani za vyuo vya ufundi stadi vya wilaya za Uyui na Igunga.

 “Nilivyojiunga kwenye huu mradi nimeweza kupata uzoefu wa kazi. Huu mradi licha ya kutupatia kipato, unatusaidia sana wanafunzi na wahitimu wa VETA kupata uzoefu na umahiri wa kazi, hata baada ya kutoka hapa tunaweza kufanya kazi mbalimbali kwa kujiamini na kwa ubora zaidi,” anasema.

Katika utekelezaji wa mradi huu zaidi ya ajira 15,000 zimetolewa kwa wananchi walioko katika maeneo ambako mradi umekelezwa. Makundi yaliyonufaika na ajira hizo ni pamoja na; Mafundi, vibarua, baba na mama lishe, huduma za ulinzi, na wazabuni mbalimbali. Vyuo vitakapoanza kutoa mafunzo inatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 1000 na kukuza uchumi maeneo ya jirani.

Vilevile wahitimu wa shahada za uhandisi ambao ni watumishi wa VETA waliweza kupata uzoefu wa kusimamia miradi, jambo ambalo limechangia pia baadhi yao kukidhi vigezo vya kusajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB).

 Ujenzi wa vyuo hivyo umepongezwa na kupokelewa kwa furaha na viongozi na wananchi wa makundi mbalimbali katika wilaya husika.

Kanali Denis Filangila Mwila, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe anasema kuwa ni fursa kubwa kwa vijana na wananchi wa Ukerewe, kwani kisiwa hicho kina mahitaji makubwa ya ujuzi na ni muhimu kwa baadhi ya wananchi ambao wanalazimika kutoka kwenda maeneo mengine kutokana na ongezeko la watu kwenye kisiwa hicho.


“Ukerewe ni miongoni mwa sehemu zenye idadi kubwa ya watu. Kwa vyovyote vile hawa watu lazima watoke kwa sababu ardhi ni ndogo na watu wanazidi kuongezeka. Ili watoke ndani ya Ukerewe, ni vizuri wakitoka wakiwa na ujuzi mbalimbali. Kwa hiyo tunaishukuru sana VETA kwa kutuletea chuo hiki. Kitawapa mafunzo ya kozi mbalimbali vijana na watatoka wakiwa na ujuzi kwenda kutafuta kazi sehemu zingine,” amesema.

Pia Kanali Mwila akaishauri VETA kuanzisha kozi zinazohusiana na uvuvi, ufugaji wa samaki na utengenezaji mitumbwi ili kwenda sambamba na shughuli za kiuchumi za wilaya ya Ukerewe.

Mzee Peter Nyamko, kutoka kijiji cha Butiama, wilayani Butiama anasema, “Mama Samia, Mheshimiwa Rais wetu ametilia mkazo sana hivi vyuo. Ajuaye uchungu wa mwana ni mama. Mama amekuja na nguvu mpya, akisema lazima nioneshe watoto wetu wanasoma, na ndio maana akasema afungue hivi vyuo vingi ilia one maendeleo yake. Na mimi namshukuru na Taifa litamshukuru kwa kazi kubwa anayoifanya.”

Katika kipindi cha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa vyuo 25 vya ufundi stadi vya wilaya, VETA iliendelea pia kuratibu, usimamizi na ufuatiliaji wa ujenzi wa vyuo vinne (Kasulu, Kongwa, Nyasa na Ruangwa) ambavyo vilikuwa vikijengwa na halmashauri husika; ujenzi wa vyuo vitano vya VETA vya ngazi ya mkoa, katika mikoa ya Simiyu, Geita, Rukwa, Njombe na Kagera.

Ukamilishaji wa vyuo vya VETA vya mikoa ya Simiyu, Geita, Rukwa na Njombe unafanyika kwa fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, ambapo serikali ilitenga shilingi bilioni 18.70 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na kuweka samani katika vyuo hivyo. Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera kimejengwa kwa msaada wa serikali ya China na kimeshakamilika. Serikali pia ilitoa bilioni 1.04 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa mabweni katika Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro, lengo likiwa ni kuongeza fursa za mafunzo ya Ualimu wa ufundi stadi ili kuendana na ongezeko la vyuo vya ufundi stadi nchini.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Kasore anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutambua umuhimu wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi na kuyapa kipaumbele kikubwa.

“Vyuo vinavyojengwa vitawapa vijana fursa ya mafunzo kwa vitendo ili wapate ujuzi stahiki utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika ukuzaji wa uchumi wa nchi,” anafafanua.

Vilevile anaishukuru Serikali, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuiamini VETA na kuipa jukumu muhimu la kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 25 nchini kwa kutumia utaratibu wa Nguvu Kazi ya Ndani ya VETA (Force Account) na kubainisha kuwa mafanikio hayo yanaakisi utekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano unaomalizika katika mwaka wa fedha 2022/2023 uliokuwa na lengo mahsusi la kuongeza upatikanaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa makundi yote nchini.

 




No comments:

Post a Comment