CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Thursday 23 May 2024

KAMPUNI YA SAINT PARTS YAIPATIA VETA INJINI ZA KUFUNDISHIA

 

Kampuni ya Kijapan ya Saint Parts ya kutengeneza magari nchini imeipatia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) injini Nne za kufundishia fani ya ufundi magari kwa ajili ya kuimarisha utoaji mafunzo katika vyuo vya VETA.

Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo, leo tarehe 24 Mei, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema vifaa  hivyo vitachangia kuimarisha utoaji mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi kuendana na ukuaji wa teknolojia ya magari inayobadilika kila mara huku Tanzania ikiwa ni watumiaji wakubwa wa magari ya  Kijapan.

CPA Kasore amesema VETA kupitia vyuo vyake nchini imejidhatiti katika kutoa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya soko la ajira na kuishukuru kampuni hiyo kwa kuwezesha vifaa hivyo muhimu kwa mafunzo ya ufundi wa magari.

Meneja Masoko wa Kampuni ya Saint Parts, Kanya Phiri, amesema kuwa wameguswa kutoa vifaa hivyo kwa lengo la kuongeza wigo wa utoaji mafunzo ya ufundi magari kwa vijana wa Kitanzania.

Phiri  amesema kuwa kutokana na uwepo wa magari mengi ya Kijapan hapa nchini, uhitaji wa mafundi wa kuhudumia magari hayo ni mkubwa na kwamba ni fursa ya kuongeza ajira kwa vijana kwenye eneo la ufundi magari.

Aidha amesema kuwa Kampuni hiyo itashirikiana na chuo cha VETA Dar es Salaam na Vyuo vingine vya VETA nchini kwa kutoa fursa ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi na walimu ili kuwawezesha kubobea kwenye eneo la ufundi wa magari.

Mwanafunzi wa Fani ya Umeme wa Magari, Halima Mabrouk amesema kuwa msaada huo ni muhimu kwao katika kuendeleza ujuzi wa utengenezaji wa magari katika mifumo yote.

Amewahamasisha wasichana kutumia fursa ya mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na vyuo vya VETA kujipatia ujuzi.

No comments:

Post a Comment