Kwa kutambua umuhimu wa Ubunifu kama nguzo muhimu katika kuboresha mafunzo ya ufundi stadi na mahitajio halisi ya soko la ajira, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imepanga kuanzisha Klabu za Ubunifu katika vyuo vyake nchini.
Lengo la kuanzisha Klabu hizo ni kutaka kukuza uwezo wa wanafunzi na Wakufunzi katika utatuzi wa matatizo kwa njia ya kibunifu, kuendeleza mawazo mapya na kutumia maarifa yao kutatua changamoto za jamii kiuhalisia.
Katika kutekeleza mpango huu, VETA imeitisha kikao cha siku nne kuanzia tarehe 11 Juni, 2025 katika ukumbi wa Mt. Gaspar jijini Dodoma ikihusisha wadau muhimu katika maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ili kuwasilisha mpango wa kuanzisha Klabu, kubadilishana uzoefu na kuandaa mpango kazi wa utekelezaji.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony Kasore amesema,
katika dunia ya sasa ubunifu ni kitu cha lazima ili kutatua changamoto mbalimbali
zilizopo katika jamii hivyo kuna haja ya kuwajengea watu uwezo wa kibunifu.
Amesema, kupitia Klabu za Ubunifu, vijana watachochewa kubuni, kuwa wajasiriamali, kusimamia bunifu zao katika kukuza na kuchochea maendeleo yao binafsi kwa kuanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa za ndani badala ya kutegemea kutoka nje.
Amesema, sambamba na mpango wa Klabu za Ubunifu, VETA imeanzisha kampuni ambayo itaingia makubaliano na wabunifu mbalimbali wanaozalisha bidhaa ili kuzizalisha kwa wingi na kuziusa na kuziuza.
CPA. Kasore ameongeza
kuwa, kila mwaka zaidi ya vijana zaidi ya elfu sitini (60,000) wanapata mafunzo
katika vyuo vya VETA nchini, hivyo kuna haja ya kuwajenga uwezo na
kuwatengenezea mazingira wezeshi ya kiubunifu ili waweze kuzalisha bidhaa kulingana
na mahitaji ya jamii husika.