CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Thursday 29 November 2018

VETA Kihonda chaanzisha mafunzo ya mchana kukabiliana na uhitaji mkubwa wa mafunzo


Katika harakati za kukabiliana na changamoto ya mahitaji makubwa ya mafunzo ya ufundi stadi, Chuo cha VETA Kihonda mkoani Morogoro kimeanzisha masomo ya mchana kwa wanafunzi wa fani za umeme wa magari, umeme wa majumbani, ufundi wa magari, ufundi wa bomba na ukerezaji wa vyuma.

Makamu Mkuu wa chuo hicho Kashindye Maganga alieleza hayo wakati wa mahafali ya 29 ya chuo hicho yaliyofanyika Novemba 23 mwaka huu yakihusisha wahitimu wapatao 297 miongoni mwao wasichana ni 248 na wavulana ni 49.

Alisema lengo ni kuhakikisha vijana wengi zaidi wananufaika na mafunzo yanayotolewa chuoni hapo na kwamba wameanza na fani zenye uhitaji mkubwa zaidi.

Akielezea mafanikio ya chuo hicho, Mganga alisema kuwa hicho kimeweza kuongezeka udahili wa wanafunzi wa kozi ndefu kutoka idadi ya wanafunzi 480 hadi 600 kwa mwaka, huku udahili wa kozi fupi ukiongezekana kutoka wanafunzi 970 mwaka hadi 1,200 mwaka huu.

Mkuu huyo pia aliishukuru serikali kwa kuweza kuwapatia vifaa na mitambo ya kisasa ya  kufundishia fani ya Kilimo (Agro-Mechanics) na kuahidi kuvitumia kwa uhangalifu kwa ajili kufundisha wanafunzi na  kufanya uzalishaji wa mazao mbalimbali chuoni hapo.

Mjumbe wa bodi ya VETA Kanda ya Mashariki Beda Marwa aliwataka wanafunzi kutumia vyema elimu na ujuzi walioupata katika kubuni na kuzalisha bidhaa mbalimbali zitakazowatofautisha wao na wataalam wengine walioko kwenye soko ili kuweza kumudu mazingira ya ushindani.

Alisema taifa linatambua umuhimu wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika kuandaa wataalamu katika nyanja mbalimbali za ufundi ambao wanaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.

Naye Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Mashariki, Geofrey Sabuni aliwapongeza vijana kwa kuhitimu katika chuo hicho na kuwataka kuwa mabalozi wazuri wa elimu ya ufundi stadi huko wanakoenda ili kuhamasisha vijana wengi zaidi kujiunga na mafunzo hayo na kuweza kujipatia ujuzi.

Sabuni alisema  VETA  itaendelea na jitihada  za kuhakikisha inaandaa nguvu kazi mahiri kwa kuhakikisha inaandaa mitaala inayoendana na mahitaji ya soko pamoja na kuhakikisha vyuo vyake vinakuwa na walimu mahiri na wa kutosha pamoja na vitendea kazi. 



No comments:

Post a Comment