Vijana 350
wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya Ufundi Stadi katika chuo cha VETA-Tanga
kama sehemu ya kukiandaa chuo hicho kuwa kitovu cha umahiri katika utoaji
mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Vijana hao wanatarajiwa kupata mafunzo hayo kupitia mradi wa INCLU-CITIES unaotekelezwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ubelgiji (ENABEL) wakishirikiana na chuo cha VETA-Tanga.
Tarehe 10 Juni, 2025 katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha VETA cha mkoa wa Tanga.
Akizindua mradi huo kupitia kikao kazi cha wadau leo, tarehe 10 Juni 2025, Mkuu wa mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt.Batilda Salha Buriani ameipongeza VETA kwa kuendelea kuwaandaa vijana kuwa na ujuzi bora wa kuweza kuajiriwa au kujiajiri katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayopatikana na inayoanzishwa katika jiji la Tanga.
“tunaishukuru VETA kwa kushirikiana na ENABEL kuzindua na kukubali kutekeleza mradi huu ambao kupitia mafunzo yatakayotolewa tutawakomboa vijana kwa kuwapa maarifa ya jinsi ya kumudu mazingira yao,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha VETA Tanga, Gideon Ole Lairumbe amesema kuwa vijana hao 350 watatoka katika kata mbalimbali za mkoa wa Tanga ambapo vijana 150 watakuwa wale ambao hawakuwahi kuwa na ujuzi wowote, 150 ni wenye ujuzi katika sekta mbalimbali, lakini wana mapungufu kadha wa kadha katika utendaji wao, hivyo watapatiwa mafunzo yatakayowasaidia kurekebisha mapungufu hayo.
Ameongeza kuwa 50 ni
wale ambao wamepata mafunzo nje ya mfumo rasmi wa utoaji mafunzo, hivyo
watafanyiwa tathmini na kurasimishiwa ujuzi wao.
Mratibu wa Mafunzo kutoka Mradi wa INCLU-CITIES Bw. Thomas Kakurwa amesema mbali na kutoa Mafunzo kwa vijana hao 350, mradi huo utasaidia kuwajengea uwezo walimu watakaofundisha katika fani husika ambazo ni Uandaji wa chakula, Uvuvi, Umeme jua, Uungaji na uundaji vyuma, matengenezo ya pikipiki za umeme na simu za mkononi pamoja na kuboresha na kununua vifaa vya kufundishia katika karakana.
Mradi wa INCLU-CITIES
umekwishaanza kutekelezwa kwa hatua za awali katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Pemba
kutoka Aprili, 2025 na unatarajiwa kukamilika Septemba, 2026.
No comments:
Post a Comment