CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 2849 Dar es Salaam, Tanzania. E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 22 2863409 / Fax: +255 22 28 63408 / Url: www.veta.go.tz

Friday, 17 January 2020

Shiriki MAKISATU 2020Je wewe ni Mbunifu wa Teknolojia au suala lolote la Kisayansi au Maarifa Asilia?Karibu ushiriki katika Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU).


Kuhusu MAKISATU: Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) yameanzishwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kutambua, kuendeleza na kubiasharisha ubunifu katika sayansi na teknolojia ili kuchangia katika kufikia lengo la Tanzania  kuwa nchi ya uchumi wa kati unaoendeshwa na viwanda.

Kaulimbiu na Kilele cha MAKISATU 2020:  Mashindano hayo yanafanyika mwaka huu yakiwa na Kaulimbiu, “Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Uchumi wa Viwanda” na kilele chake kinatarajiwa kufanyika Dodoma mwezi Machi.  

Uratibu wa VETA:  Katika Mashindano hayo, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) inaratibu mchakato wa mashindano katika ngazi ya Vyuo vya Ufundi Stadi na Sekta Isiyo Rasmi.

Shiriki mashindano: VETA inawakaribisha wabunifu wa Teknolojia na masuala ya Kisayansi au Maarifa Asilia walio kwenye Vyuo vya Ufundi Stadi au Sekta Isiyo Rasmi kushiriki mashindano hayo.  

Mwisho wa kuwasilisha fomu za maombi ni tarehe 31 Januari 2020. Pakua hapaMwongozo na Fomu kwa ajili ya Mashindano hayo.

Kwa maelezo zaidi au ufafanuzi, piga simu au tuma ujumbe kwenda 0736505027 au 0755267489 au Barua pepe pr@veta.go.tz

Thursday, 9 January 2020

VETA, Wizara ya Kilimo zaingia makubaliano kudhibiti Sumukuvu


Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesaini makubaliano na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Kudhibiti Sumukuvu nchini Tanzania, kwa Kiingereza "Tanzania Initiatives for Preventing Aflatoxin Contamination (TANIPAC)".

Makubaliano hayo yametiwa saini leo kati ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe, aliyewakilishwa kwenye hafla hiyo na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Kilimo, Bi. Hilda Kinanga.

Jukumu la VETA katika mradi wa TANIPAC ni kutoa mafunzo kwa vijana 400 katika kutayarisha vihenge vya chuma (metal silos) kwa ajili ya kuhifadhia mazao.

Mradi huo utakaotekelezwa kwa miaka mitano, kuanzia 2019 hadi 2023 unalenga kushughulikia changamoto ya usalama wa chakula, hususani Sumukuvu, katika mnyororo wa thamani wa mazao ya karanga na mahindi. 

Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Bujulu, amesema VETA imelipokea jukumu hilo kama fursa ya kipekee, kwani ingawa imekuwa ikitoa mafunzo kwenye fani mbalimbali za kilimo, ni mara ya kwanza kupewa jukumu maalum kwa ajili ya mafunzo ya utengenezaji wa vihenge (silos).

_“Tuko tayari kutoa mafunzo hayo kwa hao vijana 400 waliolengwa na mradi huu ambao watakuwa chachu katika kusambaza teknolojia hiyo nchini. Lakini hatutaishia hapo tu, bali tutatoa kwa Watanzania wengine watakaohitaji mafunzo hayo ili kusaidia kulinda afya za walaji na kuongeza tija kwenye kilimo,”_ Dkt. Bujulu amefafanua zaidi.

Kwa upande wake Bi. Kinanga ameishukuru VETA kwa kukubali ushirikiano huo na kueleza kuwa ana matumaini kuwa ushirikiano huo utaweza kuleta matokeo yaliyotarajiwa.

Thursday, 19 December 2019

VETA, Henan-China kujenga chuo mahsusi katika fani za Kilimo na Mifugo


Kwa kuzingatia mahitaji ya ujuzi kwenye sekta za Kilimo na Mifugo, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) iko katika hatua za juu za majadiliano na Chuo cha Ufundi Stadi wa Kilimo Henan cha nchini China kwa lengo la kuanzisha chuo maalum cha ufundi stadi kitakachobobea katika utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi katika fani za Kilimo na Mifugo.

Ujumbe wa timu ya viongozi na wataalam 9 kutoka Chuo cha Henan, ukiongozwa na Makamu wa Rais wa Chuo hicho, Prof. Wu Guozhao, umekuwepo nchini kwa siku mbili, tarehe 18 na 19 Desemba 2019 kwa ajili ya kutembelea vyuo vya VETA na kufanya mazungumzo ya awali na Menejimenti ya VETA juu ya mpango huo. Timu hiyo ilitembelea na kujionea mazingira na hali halisi ya utoaji mafunzo katika vyuo vya VETA Kihonda kinachotoa mafunzo katika Fani ya Ufundi wa Zana za Kilimo na Chuo cha TEHAMA cha VETA Kipawa.  Ikiwa Morogoro, timu hiyo ilipata pia fursa ya kutembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa lengo la kupanua zaidi ufahamu wa mafunzo ya kilimo yanavyotolewa nchini.

Akizungumzia wakati wa majadiliano na ujumbe huo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu amesema ana imani kubwa kuwa mpango wa ujenzi wa chuo hicho utawavutia wengi na unagusa sekta ya kipaumbele kikubwa katika jamii.

Alisema asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi kwa kutegemea kilimo na hata wafanyakazi na wafanyabiashara wengi nchini pia wanapenda kujishughulisha na kilimo.

“Mathalani, kwa miaka mingi watu wengi wanaulizia mafunzo ya Kilimo cha Mazao ya Bustani, Usindikaji wa Mazao ya Chakula na hata Kilimo cha Mazao ya Nafaka. Kwa ujumla naona kuna mahitaji mengi ya ujuzi katika eneo la kilimo. Bila shaka mpango huu utaungwa mkono na Serikali yetu tukufu ya awamu ya tano,” alisema Dkt. Bujulu.

Alisema VETA ina nia ya kuimarisha mafunzo katika sekta ya Kilimo na Mifugo na miongoni mwa malengo ni kuwa na chuo mahsusi kitakachobobea na kuwa kituo bora cha mfano katika mafunzo ya ufundi stadi kwenye sekta za Kilimo na Mifugo.

Katika vyuo vinavyomilikiwa na VETA, mafunzo ya muda mrefu ya ufundi stadi yanayogusa sekta ya kilimo hutolewa katika fani za Ufundi wa Zana za Kilimo (VETA Kihonda, VETA Manyara, VETA Arusha-Oljoro, VETA Mpanda na VETA Dakawa); Ufugaji (VETA Singida); Teknolojia ya Usindikaji wa Nyama (VETA Dodoma). Vilevile VETA huendesha kozi za muda mfupi ambazo ni za kati ya miezi miwili hadi sita kupitia programu yake ya Uboreshaji Ujuzi kwa Wajasiriamali kwenye Sekta Isiyo Rasmi (INTEP) ukihusisha mafunzo mbaimbali kama Kilimo cha Uyoga, Ufugaji wa Samaki, Utengenezaji Mvinyo, Usindikaji wa Mboga na Matunda, Usindikaji wa Samaki na Usindikaji wa Asali.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Chuo cha Henan, Wu Guozhao amesema ni vyema kuweka mpango maalum wa utekelezaji wa wazo hilo la kujenga chuo kwa ushirikiano na kuhakikisha kuwa pande mbili zinauridhia kabla ya kuanza kuutekeleza hatua kwa hatua.

“Hata sisi tunahitaji ridhaa ya Serikali yetu. Chuo chetu kinaendeshwa kwa fedha za serikali, tunaweza kupata msaada wa serikali kwa kiwango fulani. VETA nanyi mnapaswa kuzungumza na serikali ili kupata ridhaa yake na kuomba ufadhili kwa ajili ya ujenzi na uendeshaji wa chuo hicho,” amesema Guozhao.

Ameongeza chuo cha Henan kitatumia uzoefu wake katika mafunzo mbalimbali kwenye eneo la Kilimo na kushirikiana na  VETA katika kubuni na kuanzisha kozi ambazo zitawiana na mahitaji ya Watanzania.

Mazungumzo hayo yamehitimishwa kwa makubaliano ya VETA kuandaa Andiko la Mradi wa Chuo cha Ufundi Stadi wa Kilimo na kuainisha na kuliwasilisha kwa Serikali ya Tanzania ili kupata ridhaa yake, kabla ya hatua zingine za majadiliano ya utekelezaji kuendelea.

Miongoni mwa mambo ambayo Andiko hilo linapaswa kuainisha ni muundo utekelezaji wa majukumu na ushiriki wa pande zote mbili (yaani Chuo cha Henan na VETA) katika gharama za ujenzi; ununuzi wa vifaa; uandaaji wa mitaala; muundo wa fani; utungaji mitihani na utoaji vyeti na usimamizi wa chuo. Vilevile, imekubalika kuwa Andiko linatakiwa kupendekeza mahali pa kujenga chuo kwa kuzingatia vigezo mbalimbali pamoja na kuainisha kozi zitakazofundishwa na utaratibu wa kuanza kwa kozi hizo hatua kwa hatua.

Tayari VETA na Henan zilishasaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) katika maeneo mbalimbali ya utoaji mafunzo na uendelezaji ujuzi tangu Desemba mwaka jana na hatua mbalimbali za utekelezaji wa MoU hiyo zimeshafanyika ikiwa ni pamoja na kutembeleana na kubadilishana uzoefu.

Miongoni mwa matunda ya hivi karibuni ya makubaliano ufadhili na Chuo cha Henan kwa walimu 10 kutoka vyuo mbalimbali vya ufundi stadi kujiunga na mafunzo ya miaka mitatu katika fani mbalimbali za kilimo katika chuo hicho nchini China. Walimu hao wataondoka mapema Februari 2020 kwa ajili ya kwenda kuanza masomo.

Chuo cha Henan cha Ufundi Stadi wa Kilimo (Henan Vocational College of Agriculture) kilianzishwa mwaka 1952. Chuo hicho kilichopo katika jimbo la Henan kinachomilikiwa na serikali ya China ni chuo cha mfano katika utoaji wa elimu ya ufundi stadi katika fani mbalimbali za kilimo ikiwa ni pamoja na kilimo cha bustani na mbogamboga, ufugaji na usindikaji wa chakula.


Wednesday, 18 December 2019

VETA kushirikiana na Wadau wa hoteli Mtwara na Lindi kutoa mafunzo ya Uanagenzi


Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imekutana na wadau wa sekta ya Hoteli (Ukarimu) na Utalii wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kuweka mikakati ya kuanza kutoa mafunzo kwa ushirikiano kupitia programu ya Uwanagenzi Pacha (Dual Apprenticeship training).

Akifungua warsha hiyo mkoani Mtwara Desemba 17, 2019, Mkuu wa Chuo cha VETA Mtwara Ndugu Joseph Kibehele amesema utoaji mafunzo kupitia programu hiyo unategemea sana wenye viwanda, kampuni na hoteli kushiriki kikamilifu.

“Tunawaomba sana mshiriki katika programu hii ili tuweze kuandaa wafanyakazi wenye viwango mnavyovihitaji kwenye hoteli zenu.”Alisema
 Aliongeza kuwa VETA inatambua umuhimu wa kushirikiana na viwanda katika kutoa mafunzo kwa kuwa ushirikiano huo unawezesha kuandaa nguvu kazi mahiri zaidi inayoendana na mahitaji halisi ya viwanda hasa kwa kuzingatia kuwa sehemu kubwa ya mafunzo hayo yanafanyika sehemu za kazi.


Mratibu wa programu hiyo Ndugu. Francis Komba alisema kuwa VETA imeamua kutoa mafunzo ya Uanagenzi pacha katika sekta hiyo kupitia mfumo huo baada ya Utafiti wa soko la ajira kufanyika katika mikoa hiyo na kubaini mahitaji makubwa ya wataalamu wa hoteli na utalii kwa ngazi ya ufundi stadi.

Alisema mafunzo katika programu hiyo kwa mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye fani ya Ukarimu na Utalii yanatarajiwa kuanza kutolewa mwezi Januari, 2020 kupitia chuo cha VETA Mtwara.

Kwa mujibu wa Komba, mafunzo kupitia programu hiyo yanamwezesha kijana kupata ujuzi wa fani husika akiwa chuoni na sehemu ya kazi, hivyo kumwezesha kwa kiasi kikubwa kujifunza kwa vitendo na kuendana na mahitaji ya soko la ajira pamoja na kupata uzoefu na uelewa wa mazingira halisi ya kufanyia kazi.

Meneja wa Shangani Apartments Ndugu Athumani Akida amesema kuwa mfumo huo wa mafunzo utasaidia wenye hoteli kupata wafanyakazi bora zaidi kwa kuwa wenye hoteli wanapata fursa ya kushiriki kuwandaa wakati wa mafunzo. Alisema “Naamini kabisa programu hii itaondoa lile gap linalojitokeza kati ya sisi waajiri na wanafunzi wanaozalishwa vyuoni”.

Naye Afisa Mwandamizi wa hoteli ya BNN Royal Palm Bi. Grace Paul alisema kuwa hoteli yake iko tayari kushiriki kikamilifu katika kutoa mafunzo hayo na kushauri wadau wengine kujitokeza kushiriki kutoa mafunzo kupitia programu hiyo yenye faida kwao.

Mratibu msaidizi wa programu hiyo Ndugu Fahil Challange alisema kuwa  hadi kufika mwaka 2023 VETA inatarajia kuzalisha wahitimu 15,000 kupitia programu hiyo kutoka 500 wa sasa na kuongeza fani hadi kufikia tisa kutoka tano zilizoko sasa kutokana na mpango kazi ambao VETA imeandaa kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Chama cha Waajiri Tanzania ATE.

Mfumo wa utoaji mafunzo ya Uanagenzi pacha unahusisha kuhudhuria mafunzo ya vitendo kwenye karakana na darasani (VETA) na kufanya vitendo zaidi katika sehemu za kazi. Mafunzo hayo ni ya miaka mitatu ambapo kwa kila mwaka mwanagenzi anatumia wiki 20 VETA na wiki 32 kwa mafunzo ya viwandani.

Mfumo wa mafunzo ya Uanagenzi pacha ulianzishwa mwaka 2011/12 kwa ushirikiano kati ya VETA na Hamburg Chamber of Skills Craft ya Ujerumani ambapo kwa sasa unatekelezwa katika vyuo vinne vya VETA vya Moshi (Ukarimu na Utalii), Dar es Salaam (Ufundi Umeme na Ufundi Magari), Simanjiro (ufundi ujenzi) na Manyara (Ufundi wa zana za kilimo).Friday, 13 December 2019

Ufundi Stadi Kufundishwa kwa Lugha ya Kiswahili


Katika lengo la kuendelea kupanua wigo na fursa za upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetafsiri Mitaala ya fani 24 na Mihtasari 16 katika lugha ya Kiswahili.

Mitaala na Mihtasari hiyo imekabidhiwa rasmi leo, tarehe 13 Desemba, 2019 kwa Naibu Katibu Mkuu (E), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu, na inatarajiwa kuanza kutumika kufundishia ufundi stadi katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) nchini. 

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo kwenye ofisi za VETA Makao Makuu Jijini Dar es Salaam, Dkt. Semakafu aliipongeza VETA kwa kukamilisha kazi hiyo na kusema kuwa ufundishaji kwa Kiswahili kutawawezesha wananchi wengi, kujifunza na kuelewa vyema mafunzo hayo.

Alisema, wapo watu wengi walioamua kujifunza ufundi stadi katika mfumo usio rasmi kwa sababu ya changamoto ya lugha inayotumika kufundishia, kwani wengi wao wana ugumu kufuatilia vyema mafunzo yanayotolewa kwa lugha ya Kiingereza.  

“Tunakwenda kwenye Uchumi wa Viwanda. Inabidi tukubali kubadilika. Matumizi ya Mitaala ya Kiswahili iwe hatua ya kwanza. Kuna mengi ya kuboresha. Tufungue milango ili tupokee mawazo mapya na kuyafanyia kazi. Ufundi Stadi uwe mkombozi kwa jamii nzima ya Watanzania, hata wanaoendesha shughuli zao za kifundi mitaani,” alisema Dkt. Semakafu.

Aliishauri VETA kuchambua na kuona kama kuna haja ya kuwa na kundi la wale wanaotaka kujifunza kwa Kiingereza kwa lengo la kuendelea na masomo ya juu zaidi, lakini mafunzo ya jumla yatolewe kwa lugha ya Kiswahili. 

Akitoa taarifa kwa Naibu Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu alisema jumla Mitaala 24 na Mihtasari 16 imetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, ambapo nakala 240 zimechapishwa kwa kila kitabu, hivyo kufanya jumla ya nakala za Mitaala na Mihtasari zilizoshachapwa kuwa 9,600.