Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Dar es Salaam imepokea magari tisa yaliyotumika kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF) kwa ajili ya kuendeshea mafunzo.
Akikabidhi magari hayo Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Shirika la EGPAF Bi Jacquesdol Massawe alisema kuwa EGPAF imewiwa kutoa msaada wa magari hayo kwa VETA ili kuwezesha uboreshaji wa mafunzo katika vyuo vya Ufundi Stadi.
Alisema
shirika lake linatambua mchango mkubwa wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa
taifa kwa kuwa vijana wengi wamekuwa wakifaidika na mafunzo hayo ambayo
yanawawezesha kwa kiasi kikubwa kuajirika.
Alisema
mahusiano mazuri kati ya VETA na EGPAF yanatarajiwa kuzaa matunda mengi zaidi
na kwamba shirika lake litaendeleza ushirikiano huo ili kunufaisha vijana wengi
zaidi.
Mkurugenzi
wa VETA Kanda ya Dar es Salaam Habibu Bukko alisema kuwa magari hayo yamekuja
wakati mwafaka ambapo VETA inakabiliwa na upungufu wa magari kwa ajili ya
kufundishia na kwamba upungufu huo unasababishwa na Sheria za Manunuzi ambazo
haziruhusu ununuzi wa magari yaliyotumika.
Alisema
magari hayo yanayokadiriwa kuwa na thamani ya Shilingi Milioni 90 yatapunguza
kwa kiasi kikubwa uhaba uliopo na hivyo kuboresha utoaji wa mafunzo katika fani
zinazohusiana na magari.
Bukko
aliwaomba wadau mbalimbali kushirikiana na VETA katika kufanikisha juhudi zake
za utoaji wa mafunzo bora kwa kusaidia vifaa mbalimbali vya utoaji mafunzo na
kwamba misaada inayohitajika si magari pekee.
Akitoa
shukrani zake kwa shirika hilo, Mkuu wa Chuo cha VETA Dar es Salaam Douglas
Kipokola alisema chuo chake kitahakikisha kuwa magari hayo yanatumika kikamilifu
kuongeza wigo wa utoaji mafunzo hasa kwa fani ya udereva na ufundi magari.
Alisema
mgao wa magari ambayo chuo chake kitapewa utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza
udahili wa wanafunzi wa udereva. EGPAF - Tanzania
No comments:
Post a Comment