Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imekisaidia chuo cha
Ufundi kwa Watu wenye Ulemavu Yombo vifaa mbalimbali vya kufundishia vyenye
thamani ya shilingi mil 41.4.
Akikabidhi vifaa hivyo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi Stadi Kanda ya Dar es Salaam Dkt. Patricia Mwesiga alisema
utoaji wa vifaa hivyo ni utekelezaji wa moja ya jukumu la VETA la kugharamia
utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo mbalimbali inavyovisimamia
nchini.
Alisema vifaa hivyo vimetolewa ili
kuboresha utoaji wa mafunzo na kuongeza udahili kwa watu wenye ulemavu ili
kuhakikisha vijana wenye ulemavu wanapata stadi mahiri zitakazowawezesha
kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo hasa katika kujenga uchumi wa
viwanda.
Alisema serikali kupitia VETA inawathamini watu wenye ulemavu na kwamba
itaendelea kushirikiana nao bega kwa bega kuhakikisha wanatimiza malengo yao
bila kubaguliwa.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es Salaam Florence Kapinga
alivitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na vyerehani vya kuendesha kwa mkono ,
vyerehani vya kuendesha kwa mguu, mashine ya nukta nundu, mashine za kuchomelea
pamoja na vifaa vya kilimo, umeme na ujenzi vyenye thamani vitatumika katika
fani za Umeme, Ushonaji,Uashi,Uungaji vyuma,Kilimo pamoja na ufugaji ambazo
zinatolewa chuoni hapo.
Mkurugenzi huyo aliwataka wanafunzi na walimu kutumia vyema vifaa hivyo
na kuvitunza ipasavyo ili kunufaisha vijana wengi zaidi watakaosoma katika chuo
hicho.
Awali, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Yombo Mariam Chellangwa alisema
vifaa walivyopatiwa vitasaidia kwa kiwango kikubwa sana kuboresha utoaji wa
mafunzo chuoni hapo ambao umekuwa ukikabiliwa na changamoto nyingi.
Alisema chuo hicho kinakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa walimu
pamoja na miundo mbinu ya kufundishia hali inayozorotesha utoaji wa mafunzo kwa
ufanisi na kuongeza kuwa kati ya watumishi 23 wa chuo hicho idadi ya walimu ni
watano pekee.
Mkuu huyo aliiomba serikali na wadau wengine kujitokeza na kushirikiana
nao ili kuendelea kuboresha utoaji mafunzo ya ufundi stadi kwa watu wenye
ulemavu nchini na kwa kuwa chuo hicho kinategemewa na watu wenye ulemavu kutoka
nchini nzima .
Kuhusu uwezo wa udahili wa chuo hicho, Bi Chellangwa alisema chuo hicho
kina uwezo wa kutoa mafunzo kwa vijana 150 kwa mwaka japo idadi ya wanafunzi
chuoni hapo imeendelea kupungua mwaka hadi mwaka na kwa mwaka huu wana
wanafunzi 68 pekee.
Mwanafunzi wa chuo hicho katika fani ya Kilimo na Ufugaji Buga Omari
alisema vifaa walivyopatiwa vitasaidia kujifunza kwa vitendo zaidi fani hiyo na
hatimaye kukamilisha malengo yake ya kuwa mkulima na mfanyabiashara wa mazao.
No comments:
Post a Comment