Chuo
cha VETA cha Hoteli na Utalii (VHTTI)-Njiro, kilichopo jijini Arusha kiko
mbioni kuanzisha mafunzo ya utalii kwa ngazi ya stashahada na astashahada
sambamba na mafunzo yanayohusiana na mambo ya hoteli ambayo yamekuwa yakitolewa
tangu kuanzishwa kwa chuo mwaka 2011.
Hayo
yalibainishwa na Mkuu wa Chuo hicho, Christopher Ayo wakati wa mahafali ya sita
ya chuo hicho yaliyofanyika Novemba 23 mwaka huu chuoni hapo yakiwahusisha
wahitimu jumla ya wahitimu 416 wakiwemo wanaume 122 na
wanawake 294 wa mahafali ya pili (2014), ya tatu (2015), ya nne (2016) ya tano
(2017) na ya Sita (2018).
Alizitaja
kozi ambazo ziko mbioni kuanzishwa kuwa ni Uongozaji
wa Watalii na yale ya Uendeshaji na Utoaji Huduma za Kitalii na Usafiri na
kusema kuwa zimeandaliwa kwa ushirikiano na chuo cha Nova Scotia Community
College cha nchini Canada chini ya mradi wa ISTEP.
“Tayari mitaala imetengenezwa na iko kwenye hatua za mwisho kupitishwa Baraza
la Taifa la Elimu ya Ufundi-NACTE,” alisema.
Sambamba
na mpango huo, Ayo alisema kuwa chuo hicho pia kina mpango wa kuongeza udahili kutoka
220 hadi kufikia 500 kwa mwaka kwa kozi zote yaani usimamizi wa hoteli na
utalii.
Vilevile,
chuo kina mpango wa kuanzisha masomo kwa njia ya mtandao (E-learning) hasa kwa
wahitaji walio mbali na chuo wanaotaka kujiendeleza.
Ayo
aliwahamasisha wahitimu kujenga moyo wa kujiajiri ili kuweza kuzalisha na
kuajiri wengine hasa ukizingatia kuwa pamoja na kupata mafunzo katika fani zao walifundishwa
pia ujasiriamali na namna ya kutafuta masoko ya bidhaa au huduma kwa wateja.
Chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii (VHTTI)-Njiro kilianzishwa mwaka 2011 kikiwa kinatoa mafunzo ya muda mrefu na muda
mfupi katika fani za Mapokezi (Front Office Operation); Upishi (Food Production);
Huduma na Mauzo ya Vinywaji na Chakula (Food and Beverage Services and Sales);
Utunzaji, Usafi wa Nyumba na Udobi (House Keeping and Laundry Services:
Baada ya kupata usajili wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE),
kozi zilihuishwa na kuwa tatu yaani mapokezi na Huduma za Malazi (Rooms
Division); Huduma na Mauzo ya Chakula na Vinywaji (Food and Beverage Services
and Sales) pamoja na Sanaa ya Uandaaji chakula na Mapishi (Culinary Art).
Chuo hicho pia kinatoa mafunzo ya muda mfupi katika
fani mbalimbali kama Upambaji, Usafi wa majengo na maeneo ya wazi, Upishi,
Huduma ya uuzaji vinywaji, uandaaji wa keki na upambaji na mafunzo ya uongozaji
watalii.
Vilevile, Chuo kina hoteli ya kisasa yenye hadhi ya
nyota tatu (Three Stars Hotel) iliyojengwa mahsusi kwa ajili ya mafunzo ya
vitendo kwa wanafunzi.
No comments:
Post a Comment