Viongozi
wa Chuo cha VETA Cha Hoteli na Utalii-Njiro (VHTTI) wameshauriwa kubuni kozi
nyingi za muda mfupi katika nyanja za hoteli na utalii ili kunufaisha wananchi
wengi zaidi.
Ushauri
huo umetolewa Ijumaa tarehe 23 Novemba 2018 na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel
Daqarro katika mahafali ya sita ya VHTTI yaliyofanyika chuoni hapo yakihusisha jumla ya wahitimu 416 wakiwemo wanaume 122 na wanawake 294 wa mahafali
ya pili (2014), ya tatu (2015), ya nne (2016) ya tano (2017) na ya Sita (2018).
Daqarro alisema kuwa nyanja za hoteli na utalii bado zina uhitaji
mkubwa wa nguvukazi nchini hasa katika miji yenye shughuli nyingi za kiutalii
kama Arusha na maeneo ya jirani, hivyo kozi za muda mfupi zinaweza kusaidia
kupunguza changamoto ya uhaba wa watu wenye ujuzi katika nyanja hizo.
“Kupitia mafunzo ya muda mfupi chuo kitaweza kugusa na kubadilisha
maisha ya wananchi wengi ndani ya muda mfupi hususani kwa wananchi wetu wa jiji
la Arusha na maeneo jirani,” alisema.
Aliongeza kuwa kutokana na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuimarika kuna
changamoto kubwa ya kupanuka kwa wigo wa uwanja wa ajira kufuatia kufunguliwa
kwa mipaka baina ya nchi wanachama hivyo kuna fursa pia katika nchi za jirani ingawa pia
wataalamu kutoka nchi jirani wana fursa ya kuja kufanya kazi nchini.
Daqarro alieleza kufurahishwa kwake na takwimu za kuajirika kwa
wahitimu wa chuo hicho ambapo alipewa taarifa kuwa asilimia 94 ya wahitimu hao
wameshapata ajira na kwamba huo ni ushahidi wa ubora wa mafunzo yanayotolewa na
chuo hicho.
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya chuo, Mkuu wa
chuo hicho, Christopher Ayo alisema kuwa chuo hicho pia kina mpango wa kuongeza udahili
kutoka 220 hadi kufikia 500 kwa mwaka kwa kozi zote yaani usimamizi wa hoteli
na utalii. Vilevile, chuo kina mpango wa kuanzisha masomo kwa njia ya mtandao
(E-learning) hasa kwa wahitaji walio mbali na chuo wanaotaka kujiendeleza.
Chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii (VHTTI)-Njiro kilianzishwa mwaka 2011 kikiwa kinatoa mafunzo ya muda mrefu na muda
mfupi katika fani za Mapokezi (Front Office Operation); Upishi (Food
Production); Huduma na Mauzo ya Vinywaji na Chakula (Food and Beverage Services
and Sales); Utunzaji, Usafi wa Nyumba na Udobi (House Keeping and Laundry Services:
Baada ya
kupata usajili wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kozi
zilihuishwa na kuwa tatu yaani mapokezi na Huduma za Malazi (Rooms Division);
Huduma na Mauzo ya Chakula na Vinywaji (Food and Beverage Services and Sales)
pamoja na Sanaa ya Uandaaji chakula na Mapishi (Culinary Art).
Chuo hicho pia kinatoa mafunzo ya muda mfupi katika
fani mbalimbali kama Upambaji, Usafi wa majengo na maeneo ya wazi, Upishi,
Huduma ya uuzaji vinywaji, uandaaji wa keki na upambaji na mafunzo ya uongozaji
watalii.
Vilevile, Chuo kina hoteli ya kisasa yenye hadhi ya
nyota tatu (Three Stars Hotel) iliyojengwa mahsusi kwa ajili ya mafunzo ya
vitendo kwa wanafunzi.
No comments:
Post a Comment