WASICHANA nchini wameshauliwa kujiunga
na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili waweze kushiriki kikamilifu
katika kipindi hiki ambacho serikali ina mwelekeo wa kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.
Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki
na Mjumbe wa Bodi ya VETA kanda ya Mashariki Beda Marwa wakati wa Mahafali ya
29 ya Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi(VETA) Kihonda Manispaa ya
Morogoro baada ya kushuhudia idadi ndogo ya wahitimu wa kike katika mahafali hiyo.
“Jamii inatakiwa kuwahamasisha watoto
wa kike kusoma mafunzo ya ufundi stadi kwani sera ya uchumi wa viwanda
inahitaji watalamu wengi hivyo juhudi zinahitajika kuwahamasisha watoto hawa
kwa manufaa ya taifa,”alisema.
Katika mafahali hao wahitimu walikuwa
297 kati yao wavulana walikuwa ni 248 huku wasichana wakiwa 49 tu jambo ambalo
lilionekana kumsikitisha Marwa ambapo alisema jitihada zaidi zinahitajika ili uwiano
uwe sawa kwa wote.
Aidha Marwa alitawaka wahitimu wote
kuwa waaminifu na waadilifu wapatapo kazi, pamoja na kuweka malengo
mazuri ya kiuchumi kwa kuanzisha viwanda
vidogovidogo pamoja na kukemea vitendo viovu katika jamii.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa chuo
hicho Maganga Kashindye aliiomba serikali kuwasaidia kutatua changamoto ya
uhaba wa mabweni kwani yaliyopo hayajitoshelezi hivyo baadhi ya wanafunzi hulazimika
kukaa nje ya chuo na kusababisha usumbufu kwa wanafunzi wanaotoka nje ya mkoa.
Nao wahitimu wa chuo hicho waliomba kuwawezeshwa
kupata mikopo itakayowafanya kujiendeleza kiuchimi ikiwa ni pamoja na kuanzisha
viwanda hali itakayosaidia kutoa ajira kwa vijana wenzao waliokosa ajira.
No comments:
Post a Comment