Mamlaka
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeendesha semina ya kuwajengea
ufahamu jamii ya watu wenye ulemavu na kuwahamasisha kutumia fursa mbalimbali
za kujipatia ujuzi katika vyuo vya ufundi Stadi nchini ili kujikwamua kimaisha.
Akifungua semina hiyo katika ofisi za
VETA Makuu jijini Dar es Salaam Juni 21, 2019 Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt.
Pancras Bujulu amesema kuwa Mamlaka hiyo inaamini kuwa ujuzi ni nyenzo ya
msingi kabisa katika kuwawezesha watu wa makundi hayo kwenda sambamba na
wengine katika harakati za kiuchumi, hususani katika kipindi hiki cha harakati
za kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.
Alisema VETA imeendelea kubuni miradi
mbalimbali yenye kulenga katika kupanua wigo wa fursa za mafunzo ya ufundi
stadi kwa makundi maalum katika jamii, pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa
makundi hayo kupata mafunzo.
Dkt Bujulu aliwataka watu hao
kuendelea kutumia vyema fursa zilizopo za kujipatia ujuzi katika vyuo vya VETA
ili waweze kuajiriwa au kujiajiri kwa urahisi zaidi.
“Napenda nitumie
fursa hii pia kuwaomba watu mbalimbali waendelee kutuunga mkono katika
kuwezesha watu wa makundi maalum kupata mafunzo na ujuzi ili hatimaye waweze kuajirika
na hivyo kuondokana na utegemezi katika jamii.”Aliongeza
Alisema katika Mpango
Mkakati wa mwaka 2018 hadi 2023, VETA imepanga kudahili watu wenye ulemavu 400
na wenye changamoto mbalimbali za kimaisha 2,400 kila mwaka.
Mkutano huo umehusisha
washiriki 60 kutoka kwenye jamii ya wasiiona, wenye ulemavu wa viungo, viziwi
na wenye ualbino.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo Wakili Dkt.
Gideon Mandesi aliiomba VETA kuanzisha dawati maalum la watu wenye ulemavu
katika vyuo vyake vyote ili kuwezesha kundi hilo kuhudumiwa kwa ufahisi zaidi.
Naye mmoja wa
wahitimu wa kozi ya Useremala asiyeona Ndugu Boniface Kiyenze aliwasihi watu wa
jamii hiyo kujiunga na vyuo vya ufundi stadi na kujipatia ujuzi utakaowawezesha
kuendesha maisha yao kama yeye alivyofanikiwa kuendesha maisha yake na familia
yake.
Miongoni mwa mada zilizotolewa katika semina hiyo ni
Fursa za Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi;
Stadi za Ujasiriamali na Programu ya Mafunzo ya Kukuza Ujasiriamali
katika Sekta isiyo Rasmi.
Semina hiyo imetolewa kama sehemu ya Maadhimisho
ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika kitaifa kuanzia tarehe 16 hadi 23
Juni, 2019.
No comments:
Post a Comment