Hatua nyingine
imehesabika katika jitihada za kusogeza huduma za mafunzo ya ufundi stadi kwa
wananchi baada ya chuo cha ufundi stadi cha wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara
kuzinduliwa.
Uzinduzi wa chuo
hicho kilichopo katika kijiji cha Emboreet, Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro
umefanywa Jumamosi ya tarehe 19 Oktoba 2019 na Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako katika tukio ambalo lilihudhuriwa pia
na viongozi wa ngazi ya juu wa wilaya na halmashauri ya Simanjiro na wananchi
wa wilaya hiyo kwa ujumla.
Katika hotuba
iliyosomwa kwa niaba yake na Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi, Peter Maduki, Prof. Ndalichako alisema serikali inatambua umuhimu
mkubwa wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi katika maendeleo ya nchi, hasa
katika kipindi hiki cha mwelekeo wa serikali kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.
Alisema, serikali
inaendelea kujenga vyuo vya ufundi stadi na inatarajia kuwa kabla ya mwisho wa
mwaka huu vyuo vinavyomilikiwa na serikali kupitia VETA vitafikia 40, jambo
ambalo litasaidia zaidi kusogeza huduma za mafunzo ya ufundi stadi karibu na
wananchi.
“Kwa taarifa
nilizonazo ni kuwa vyuo vya VETA vya Wilaya za Nkasi, Ileje, Muleba na Itilima
vimekamilika na viko tayari kwa uzinduzi, hivyo tutavizindua muda wowote kabla
ya mwisho wa mwezi Novemba mwaka huu. Pia vyuo vya VETA vya Halmashauri za
Kilindi, Ngorongoro, Babati na Newala viko katika hatua za mwisho za
ukamilishwaji, hivyo vitazinduliwa kabla ya mwisho wa mwaka huu,” alisema.
Aliongeza kuwa ujenzi
wa vyuo vya mikoa unaendelea katika mikoa ya Rukwa na Geita na mchakato wa
kuanza ujenzi wa vyuo vya wilaya za Kongwa, Kasulu T.C., Nyasa na Ruangwa uko
katika hatua za mwisho, lengo likiwa ni
kuanza ujenzi kabla ya mwisho wa mwezi Oktoba 2019.
Aliipongeza VETA kwa
juhudi hizo kubwa za kuongeza wigo wa kuzalisha rasilimali watu yenye ujuzi
mahsusi kwa ajili ya kukuza uchumi wa Taifa na maendeleo kwa ujumla.
Maduki alitumia fursa
hiyo pia kuuomba uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kuwatumia vijana
watakaohitimu fani ya Uashi katika chuo cha VETA Simanjiro pale wanapokuwa na
miradi ya ujenzi kwa njia ya Force Account ili vijana hao waweze kunufaika na
ajira kwenye eneo lao na kuchangia katika ujenzi wa wilaya yao.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu aliyashukuru mashirika ya ECLAT
Development Foundation la Wilayani Simanjiro na Upendo la Ujerumani pamoja na
wananchi wa Wilaya ya Simanjiro kwa ujumla kwa kushiriki kwa kiasi kikubwa
katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho.
Alisema juhudi zao
zimeonesha mfano hai wa kuunga mkono kwa vitendo juhudi za kupanua wigo wa upatikanaji
wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa Watanzania.
“Wamefanya jitihada
kubwa katika ujenzi wa chuo hiki kwa awamu ya kwanza ambao umehusisha madarasa
matano; bweni moja la kulaza wanafunzi wa kike 48; nyumba ya Mwangalizi
(Matron); jiko moja; matundu 32 ya vyoo; kisima kirefu cha maji; pampu ya maji
inayoendeshwa na nguvu ya jua; matenki ya kuhifadhia maji; uzio wa seng’enge
kuzunguka chuo; mfumo wa umeme wa jua; pamoja na samani na vifaa vya kufundishia
na kujifunzia,” alisema.
Alisema, ili kuchangia
juhudi hizo, kuongeza udahili na kukiimarisha zaidi chuo hicho, VETA imeamua
kujenga bweni la wavulana lenye uwezo wa kulaza vijana 48 na nyumba ya Patron
sawasawa na lile lililojengwa kwa ajili ya wanafunzi wa kike ili kuleta uwiano
sawia wa kijinsia.
“Ujenzi huu
tunaufanya kwa fedha za serikali, (bajeti ya VETA) kwa kutumia wataalam na
mafundi wetu wa ndani, yaani Force Account na utagharimu kiasi cha Sh. milioni
82 ikiwa ni pamoja na mifumo ya umeme na maji na ununuzi wa vitanda, magodoro
na makabati ya vyumbani. Tunatarajia kuukamilisha kabla ya mwisho wa mwaka huu
wa 2019. Tutaendelea kuweka mipango na bajeti kwa kadri ya uwezo wetu ili
kukiimarisha zaidi chuo hiki ili kiwanufaishe wananchi, hususani vijana wa
wilaya hii ya Simanjiro,” alifafanua.
Alisema tayari chuo
hicho kimeshaanza kutoa mafunzo ambapo vijana 24 wamedahiliwa katika fani ya
Uashi tangu tarehe 31 Julai 2019, kati yao watatu ni wa kike.
Aliongeza kuwa VETA
imejipanga kuendelea na udahili mwezi Januari 2020 ambapo wanafunzi wengine 20
katika fani ya Uashi na 20 fani ya umeme watadahiliwa na wote kupatiwa malazi
katika mabweni ya chuoni hapo.
Naye Mwenyekiti wa
Shirika la Upendo la Ujerumani, Dkt. Fred Heimbach aliishauri VETA kutoa
kipaumbele kwa vijana wa Simanjiro inapofanya udahili wa wanafunzi kwa ajili ya
mafunzo katika chuo hicho, kwani kwa uchunguzi wake amebaini kuwa vijana wengi
wilayani humo wana uhitaji mkubwa wa mafunzo ya ufundi stadi.
Hafla hiyo pia
iliambatana na kubadilishana rasmi nyaraka za makabidhiano ya umiliki wa chuo
hicho kati ya Shirika la ECLAT la Wilayani Simanjiro, Upendo la Ujerumani na
VETA.
No comments:
Post a Comment