Wajasiriamali
na wahitimu wa ufundi stadi nchini wana fursa ya kunufaika na mikopo yenye
masharti nafuu baada ya taasisi tano nchini kuungana kwa pamoja kuwezesha
wananchi kuanzisha viwanda.
Taasisi
zilizounganisha nguvu ni Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA),
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo
(SIDO), Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na Benki ya
Azania, ambazo zimesaini kwa pamoja Makubaliano (MoU) ya kushirikiana
kuwawezesha wananchi kuanzisha viwanda vidogo na vya kati.
Makubaliano
hayo yametiwa saini tarehe 21 Februari, 2020 na Watendaji Wakuu wa Taasisi hizo
katika ofisi za NSSF Makao Makuu, Jijini Dar es Salaam.
Tayari
NSSF imetenga jumla ya Shilingi Bilioni Tano (Bil. 5) zitakazotolewa kupitia
Benki ya Azania, ambayo ndiyo itakuwa na jukumu la kukopesha wajasiriamali
wadogo na wa kati.
Katika
makubaliano hayo, VETA na SIDO zitakuwa na jukumu la kuwatambua, kuwajengea
uwezo na kuwapendekeza wajasiriamali kwa ajili ya mikopo itakayotolewa kupitia
Benki ya Azania.
Vilevile,
VETA itakuwa na majukumu ya kusimamia miradi iliyopata mikopo kupitia kwake na
kutoa mafunzo na ushauri wa kitaalam kwa wajasiriamali ili kuwasaidia kuboresha
miradi yao na kuendesha uzalishaji kwa tija na ufanisi zaidi.
Akifafanua
juu ya mikopo na utaratibu wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania,
Charles Itembe, alisema kuwa kiwango cha mikopo midogo kitaanzia Shilingi mil.
8 hadi mil. 50 na kiwango cha kati ni kilicho juu ya mil. 50 hadi mil. 500.
Katibu
Mtendaji wa NEEC ambayo ndio yenye dhamana ya uwezeshaji wananchi, Bi Beng'i
Issa, alisifu makubaliano hayo na kusema kuwa kipaumbele kitatolewa kwa viwanda
vya bidhaa ambazo hazipatikani hapa nchini na vile ambavyo vitashirikisha
wananchi wengi, kwa kuwa lengo ni kuhakikisha watanzania wengi wanashiriki
katika shughuli za kiuchumi.
Mkurugenzi
Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, alishukuru kuanzishwa kwa ushirikiano huo na
kusema kuwa VETA itahakikisha inatoa ujuzi unaostahili kwa wananchi kulingana
na viwanda husika na kwamba itasimamia vyema zoezi la kutambua wajasiriamali
hao.
Dkt
Bujulu amesema “Natoa wito kwa wananchi wenye nia ya kuanzisha viwanda
kujitokeza kwa wingi ili kuweza kutambuliwa ili watakaokidhi vigezo waweze
kupata mikopo hiyo”.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. William Erio, alisema kuwa muunganiko
huo umelenga hasa kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano za kuifanya
Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kuhakikisha wananchi wote wanapata fursa ya
kushiriki.
Alisema
kiasi hicho cha Shilingi Bilioni Tano (Bil. 5) ni kianzio tu ambapo mfuko huo
utaweza kuongeza fedha nyingine kulingana na mahitaji na ufanisi wa awamu hii
ya kwanza.
No comments:
Post a Comment