Mafundi
34,818 waliopata ujuzi kupitia mfumo usio rasmi (Wanagenzi) kutoka mikoa
mbalimbali nchini wameomba kufanyiwa tathmini na kurasimishiwa ujuzi wao
kupitia Mpango wa Urasimishaji Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi (RPL)
unaoendeshwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi (VETA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi,Vijana,
Ajira na Wenye Ulemavu.
Mratibu wa programu hiyo kutoka VETA Bwire Ally, amesema katika awamu ya tatu ya Mpango huo ulioanza kutekelezwa kuanzia mwezi Juni 2020, jumla ya wanagenzi 23,621 wamechaguliwa kufanyiwa tathmini baada ya kukidhi vigezo na kwamba tathmini itafanyika kwa awamu ikianza na wanagenzi 6,243 na 17,378 waliobaki kurasimishwa katika awamu zinazofuatia.
Amesema, VETA imeongeza fani zinazofanyiwa tathmini na
kurasimishwa kutoka tano za awali hadi kufikia kumi, zikiwa ni Ufundi Magari,
Useremala, Uashi, Uandaaji wa Chakula (Upishi) na Huduma na Mauzo ya Vinywaji,
Ushonaji, Umeme, Unyooshaji bodi za Magari, Ufundi Bomba na Uchomeleaji na
Uungaji Vyuma. Fani za awali zilikuwa ni Ufundi Magari, Useremala, Uashi,
Uandaaji wa Chakula (Upishi) na Huduma na Mauzo ya Vinywaji.
Akizungumzia Mpango huo, Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa VETA, Stella Ndimubenya
anasema, umewasadia vijana wengi kupata
kazi zenye staha na kuongeza tija mahali pa kazi.
Ametoa wito kwa vijana wenye
ujuzi katika fani mbalimbali ambao hawana vyeti vinavyotambulisha ujuzi wao
kuomba kuingia katika Mpango pale nafasi zinapotangazwa ili hatimaye waweze
kurasimisha ujuzi wao na kupata vyeti.
Mmoja wa wanagenzi katika fani
ya Mapishi kutoka katika chuo cha VETA Dar es salaam, Adrian Kahele amesema
mafunzo hayo yamemuongezea mwanga zaidi katika fani yake ya Mapishi, kwani kuna
stadi ambazo hakuwa nazo, lakini kupitia mafunzo hayo amezipata.
Mpango huo wa Urasimishaji Ujuzi
Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi(Recognition of Prior Learning) unalenga
kufanya tathmini, kurasimisha na kutunuku vyeti kwa mafundi wa fani mbalimbali
waliopata ujuzi mahala pa kazi (wanagenzi), pasipo kupitia chuoni.
Tangu kuanza kwa Mpango huo mwaka 2010 hadi 2019, jumla ya
wanagenzi 10,023 walirasimishwa ujuzi wao na kutunukiwa vyeti.
No comments:
Post a Comment