Jumla
ya mafundi 200 wa simu za mkononi katika mikoa ya Dodoma na Kigoma wanatarajia
kunufaika na Mafunzo ya Umahiri wa Ufundi wa Simu za Mkononi yatakayotolewa na
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kupitia chuo chake cha
TEHAMA VETA Kipawa.
Mpango wa mafunzo hayo yatakayotolewa kwa ufadhili wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) umezinduliwa tarehe 4 Septemba 2020 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo katika Chuo cha VETA Dodoma, jijini Dodoma.
Akizungumza katika tukio hilo, Dkt. Akwilapo amesema pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya simu za mkononi na umuhimu wake, hadi kufikia mwaka 2016 hakukuwa na mafunzo rasmi yanayotolewa kwa ajili ya kuandaa mafundi wa Simu wenye ujuzi stahiki, bali waliokuwa wakitoa huduma hiyo wamekuwa wakijifunza kwa njia zisizo rasmi, zikiwemo mitandao ya kijamii kama vile YouTube, na kujifunza kwa mafundi wenzao wenye uzoefu.
“Hali
hii imechangia kupungua kwa usalama wa vifaa hivi vinapotengenezwa na mafundi
wasiokuwa na ujuzi rasmi na hata kutishia usalama wa taarifa za watumiaji
zinazohifadhiwa kwenye simu zao,” amesema.
Amewasihi mafundi simu watakaopata fursa hiyo kuzingatia mafunzo, kwani itawasaidia kufanya kazi kwa weledi na uadilifu na kusema kuwa anaamini mafunzo hayo yatasaidia kupunguza malalamiko ya wateja kudai simu zao zimeharibiwa zaidi badala ya kutengenezwa.
“Nawapongeza mafundi wa simu kwa kuyapokea vyema na kuonesha utayari wa kushiriki kikamilifu katika mafunzo haya. Niwasihi kuwa msiishie tu kwenye kusoma kwa ajili ya kupata cheti na Leseni kutoka TCRA, bali mjikite zaidi katika kutoa huduma bora kwa watumiaji wa simu hizi na hatimaye pia kuchangia katika kurahisisha mawasiliano na kuendeleza uchumi wetu,” aliongeza.
Ametoa
wito kwa taasisi na kampuni mbalimbali, zikiwemo kampuni za simu nchini,
kushirikiana kwa karibu na VETA ili kuwezesha mafunzo haya kuwa endelevu na
hatimaye kupelekea Taifa kuwa na nguvukazi yenye ujuzi stahiki wa utoaji huduma
za simu za mkononi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, amesema Mafunzo ya Ufundi wa Simu za Mkononi ni mapya kwenye mfumo wa mafunzo ya kawaida ya VETA, lakini tangu yaanze kutolewa mwaka 2017, idadi ya waombaji imekuwa ikiongezeka kwa kasi kubwa na kwamba kanzi data zimeonesha kuwa hadi Septemba 2020 kulikuwa na jumla ya wahitaji wa mafunzo hayo 3,723.
“Tunapozindua
mafunzo haya hapa Dodoma leo, kuna zaidi ya mafundi simu 250 ambao wameomba
kupata mafunzo mkoani hapa pekee, na kati yao mafundi 100 tu ndio aliopata
fursa na sasa wanaendelea na mafunzo kwa ufadhili wa TCRA,” amesema.
Amesema baada ya kubaini uhitaji mkubwa, VETA imepanga kupanua mafunzo hayo na kuelekea katika mikoa mingine ikiwemo Manyara, Kilimanjaro, Kagera, Arusha, Mtwara, Lindi na mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Naye John Daffa, Mkurugenzi wa Leseni na Ufuatiliaji aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, amesema mafunzo watakaofuzu mafunzo hayo watakidhi vigezo vya kupatiwa leseni za uendeshaji wa ufundi wa simu za mkononi kutoka kwenye Mamlaka hiyo.
Amesema ili kudumisha ubora, usalama na kurasimisha shughuli za utengenezaji wa simu za mkononi TCRA kwa kushirikiana na VETA na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam iliona ni vyema kuandaa mtaala kwa ajili ya mafunzo maalum ya ufundi wa simu za mkononi.
No comments:
Post a Comment