CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Tuesday 15 December 2020

Mafundi 200 kunufaika na mafunzo ya umahiri wa ufundi wa simu za mkononi mkoani Arusha na Kilimanjaro

 
Jumla ya mafundi 200 wa simu za mkononi katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro wanatarajia kunufaika na mafunzo ya umahiri wa ufundi wa simu za mkononi yanayotolewa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Akizindua mafunzo hayo jijini Arusha, tarehe 4 Desemba, 2020, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Idd Hassan Kimanta, alisema mafunzo hayo ni muhimu sana katika kuandaa mafundi simu watakaofanya kazi kwa weledi na uadilifu.

Mhe. Kimanta alisema mafunzo haya yamekuja wakati mwafaka ambapo matumizi ya simu za mkononi yanaendelea kuongezeka kwa kasi kubwa na vijana wengi wanajipatia ajira kupitia shughuli za ufundi simu hivyo mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha ujuzi wao na kuweza kufanya kazi hizo kwa tija zaidi.

Mhe. Kimanta aliwataka mafundi hao kuzingatia mafunzo yatakayotolewa ili wakafanye kazi kwa weledi kwa kuhakikisha usalama wa simu watazotengeneza pamoja na usalama wa maisha ya watumiaji pamoja na mali zao.

Mafunzo hayo yanatolewa na VETA kupitia vyuo vyake vya VETA Moshi na VETA Arusha kwa uratibu wa Chuo cha Tehama VETA Kipawa, na kufadhiliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema uhitaji wa ujuzi wa ufundi simu ni mkubwa hasa ukizingatia kuwa matumizi ya simu za mkononi Tanzania yameongezeka kwa kasi kubwa ambapo hadi sasa zaidi ya simu za mikononi milioni 45 zinatumika sehemu mbalimbali nchini, na zimeenea kwa zaidi ya asilimia 65 ya Tanzania.

Dkt. Bujulu alisema kanzidata zimeonyesha kuwa kuna Watanzania zaidi ya 4,700 walioonyesha uhitaji wa mafunzo hayo ambapo asilimia 10 ni wanawake na asilimia 3 wako kwenye kundi la watu wenye uhitaji maalum. 

“Mikoa inayoongoza kwa uhitaji wa mafunzo haya ni pamoja na Dar es salaam 1,174; Dodoma 237; Kigoma 168; Arusha 116; Kilimanjaro 130; Tanga 93 na Manyara 78. Pia mikoa kama Iringa, Mtwara, Lindi, Ruvuma na Zanzibar imeonyesha uhitaji mkubwa kupata mafunzo haya,”alisema.

Alisema VETA itaendelea kuhakikisha mafunzo hayo yanatolewa kwa mafundi simu wenye uhitaji nchini kote ili kuwezesha mafundi simu kujipatia ujuzi stahiki utakaowawezesha kufanya kazi zao kwa umahiri zaidi.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Mhandisi James Kilaba alisema TCRA itaendelea kufadhili utoaji wa mafunzo hayo ili kuhakikisha mikoa yote nchini inafikiwa na mafunzo hayo muhimu.

Kwa mujibu wa Mhandisi Kilaba, mafundi watakaofuzu mafunzo hayo watakidhi vigezo vya kupatiwa leseni za uendeshaji wa ufundi wa simu za mkononi kutoka kwenye Mamlaka hiyo.

Hadi sasa  jumla ya mafundi 295 wa simu za mkononi wamekwishanufaika na mafunzo hayo ambapo 95 ni katika mkoa wa Dar es Salaam, 100 mkoa wa Dodoma na wengine 100 katika mkoa wa Kigoma. Mafunzo hayo yalizinduliwa rasmi kitaifa tarehe 4 Septemba, 2020 jijini Dodoma. 

 




No comments:

Post a Comment