Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameweka jiwe la
msingi la ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Korogwe na kuagiza
uongozi wa mkoa wa Tanga na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
kuhakikisha vijana wengi wa mkoa wa Tanga wanadahiliwa katika chuo hicho baada
ya kukamilika.
Katika hafla hiyo
iliyofanyika tarehe 15 Machi, 2021 katika eneo la Mtonga wilayani Korogwe, Mhe.
Makamu wa Rais ameutaka uongozi wa mkoa wa Tanga kusimamia kwa karibu ujenzi wa
chuo hicho ili kukamilika mapema na kuwezesha vijana wa mkoa wa Tanga kujiunga
na kupata ujuzi wa aina mbalimbali.
Amesema Tanga ni
miongoni mwa mikoa inayoshamiri kwa viwanda, hivyo kuna uhitaji wa nguvukazi
yenye ujuzi na kwamba ni vyema nguvukazi hiyo ikatokana na vijana wa mkoa huo
baada ya kuhitimu mafunzo ya ufundi stadi.
Awali akisoma taarifa
ya mradi wa ujenzi wa chuo hicho, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt.Pancras Bujulu,
amesema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa mwezi Machi, 2020 na umekadiriwa
kugharimu kiasi cha shilingi 1.6 bilioni.
Amesema mradi huo
unatekelezwa na VETA kwa kutumia nguvukazi ya ndani (Force Account) kupitia
Chuo cha VETA Kihonda kilichoko Morogoro.
Amesema chuo hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 240 kwa kozi za muda mrefu na wanafunzi 620 wa kozi za muda mfupi kwa mwaka.
No comments:
Post a Comment