Naibu Katibu Mkuu,
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Caroline Nombo, amewaelekeza
watendaji wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kutumia ubunifu
na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kukabiliana na changamoto za utoaji
wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Prof Nombo ametoa
wito huo leo, tarehe 14 Juni 2021, alipotembelea Makao Makuu ya VETA kwa nia ya
kupanua ufahamu wake juu ya shughuli zake, maendeleo na changamoto
inazokabiliana nazo.
Akitoa taarifa juu ya
shughuli za Mamlaka, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, alisema
licha ya mafanikio katika kupanua fursa na kuimarisha utoaji wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini, VETA inakabiliwa na changamoto za uhaba mkubwa
wa walimu na uchakavu wa vifaa vya mafunzo katika karakana za vyuo vyake, hasa
vyuo vikongwe.
Prof. Nombo aliipongeza VETA kwa juhudi inazofanya katika kuwawezesha Watanzania, husuani vijana, kupata ujuzi unaowapa fursa pana ya kuajiriwa au kujiajiri katika nyanja mbalimbali. “VETA ina umuhimu mkubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu. Kwa hiyo ni muhimu kujipanga vizuri ili kuhakikisha elimu tunayoitoa inakidhi mahitaji. Licha ya kuifahamisha Serikali juu ya changamoto zinazowakabili, kuweni wabunifu na shirikianeni na wadau katika kukabiliana na changamoto ili kazi iendelee,” alisema.
Sambamba na hilo,
Prof. Nombo alizungumzia umuhimu wa kuwafanya wenye viwanda kutambua kuwa wana
wajibu wa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa vijana wanaojifunza ufundi
stadi. Hii itawapa vijana wa VETA fursa ya kupata mafunzo yenye uhalisia
viwandani na kutumia teknolojia ya kisasa ili kuwezesha uzalishaji nguvukazi mahiri
kwa maendeleo ya viwanda.
Katika ziara yake,
Prof. Nombo aliambatana na Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi
Stadi Wizarani, Dkt. Noel Mbonde na Naibu Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi
anayesimamia vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC), Bi Magreth Issai.
Baada ya kuongea na Menejimenti ya VETA Makao Makuu, Naibu Katibu Mkuu alitembelea Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Dar es Salaam na Chuo cha VETA cha TEHAMA Kipawa. Katika vyuo hivyo, NKM alitembelea Karakana mbali mbali za vyuo hivyo na kujionea jinsi mafunzo kwa vitendo yanavyotolewa kwa vijana wa VETA na shughuli mbali mbali za uzalishaji zinazoendeshwa katika karakana hizo.
No comments:
Post a Comment