Mkurugenzi Mkuu wa
VETA, Dkt. Pancras Bujulu amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa
Geita, Mhe. Rosemary Staki Senyamule kwa lengo la kuimarisha utoaji wa mafunzo
ya ufundi stadi mkoani humo.
Mazungumzo hayo
yamefanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, tarehe 20 Septemba, 2021 na
yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ngazi ya Mkoa, wakiwemo Katibu Tawala
wa Mkoa wa Geita na Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoani humo. Kwa upande
wa VETA, kikao hicho kimehudhuriwa pia na Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali na
Utawala Bw. Felix Staki, Kaimu Mkurugenzi wa Fedha Bw. Anthony Kasore, Kaimu
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Ziwa Bw. Charles Kangele na Kaimu Mkuu wa Kitengo
cha Ununuzi Bi. Witness Mgimba.
Katika kikao hicho,
viongozi hao wamejadili mambo mbalimbali yanayohusu fursa za mafunzo ya Ufundi
Stadi mkoani humo, Maonyesho ya Teknolojia za Uchimbaji Madini yanayoendelea
mjini Geita, Matayarisho na ushiriki wa VETA kwenye Wiki ya Vijana
inayotarajiwa kufanyika Chato, Mkoani Geita mwezi ujao, na hatma ya Mradi wa
Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Geita uliokwama kutelezwa
tangu mwaka 2019 baada ya Serikali kuvunja mkataba kati yake na Mkandarasi
aliyekuwa akitekeleza mradi huo, kampuni ya Skywards Construction Co. Ltd.
Kupitia mazungumzo
hayo, Mhe. Senyamule ameitaka VETA kushirikiana kwa karibu na ofisi yake kwenye
utekelezaji wa majukumu hayo muhimu kwa Mkoa huo na Taifa kwa ujumla, ikiwemo
miradi mbalimbali inayotekelezwa na VETA katika mkoa wa Geita.
Naye Mkurugenzi Mkuu
wa VETA, Dkt. Bujulu, amemhakikishia Mkuu huyo wa Mkoa kuwa VETA itatoa
ushirikiano wa karibu kwa ofisi yake katika kuhakikisha wananchi wa Mkoa huo
wanapata ujuzi katika stadi mbalimbali,
hasa kwenye Sekta ya madini, kwani Sekta hiyo imebeba sehemu kubwa ya uchumi wa
Mkoa huo na wakazi wake.
No comments:
Post a Comment