Irene Thomas Ndunguru ni fundi umeme anayefanya
kazi zake jijini Mbeya baada ya kuhitimu mafunzo yake ya Fani Umeme katika Chuo
cha VETA cha Jijini Mbeya miaka nane iliyopita na kupata cheti chake cha Ufundi
Stadi Daraja la Tatu (Level III).
Irene anasema maono yake ya kuwa fundi umeme mwenye
uwezo wa kufanya kazi zake yeye mwenyewe yalianza kuonekana akiwa bado binti
mdogo alipokuwa akisoma katika shule ya msingi Ikulu iliyopo Jijini Mbeya na
kuwa mdadisi wa vifaa vya umeme ambapo pia alikuwa akijaribu kutengeneza vifaa
vinavyotumia umeme pale vinapopata hitilafu.
Alimaliza masomo yake ya Sekondari katika Shule ya
Ilomba na baada ya hapo safari rasmi ya kukamilisha ndoto yake ya kuwa fundi
umeme ilianza kwa kujiunga na Chuo cha VETA cha Jijini Mbeya.
Irene anasema kuwa VETA ilikamilisha ndoto zake kwa
kumpatia ujuzi ambao leo hii amekuwa akijivunia kwa kuwa na uwezo wa kufanya
kazi zake kwa weledi mkubwa uliopelekea hadi kuaminika na kufanya kazi kwenye
miradi mikubwa ikiwemo kuweka mtandao wa umeme katika Chuo cha VETA cha Wilaya
ya Mbarali kilichowekewa Jiwe la Msingi Agosti 8, 2022 na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
“Kati
ya mafanikio ambayo najivunia ni kufanya kazi mbalimbali zikiwemo za Serikali mfano
katika Chuo cha VETA Mbarali ambacho Mheshimwa Rais Samia Suluhu Hassan ameweka
Jiwe la Msingi hivi karibuni. Lakini pia nimefanya kazi katika jengo la
halmashauri ya Mbeya Vijijini,"amesema
"Naamini
kitu kinachopelekea mimi kuaminika kufanya kazi katika maeneo mbalimbali ni
utendaji kazi mzuri ikiwemo kumaliza kazi kwa wakati katika ule muda unaotakiwa
kwa kuzingatia ubora," amesema Irene
Anaongeza kwa kusema kuwa VETA imekuwa kama Mlezi
katika maisha yake kwa kumuimarisha na kumshika mkono ukiachia mbali ujuzi
aliopata lakini bado ameendelea kufanya kazi mbalimbali za taasisi hiyo.
"Kwangu
mimi VETA ni mzazi maana tangu nimefika chuoni mpaka namaliza masomo yangu
katika ngazi zote nilizopita wamekuwa wakinishika mkono hata kufikia kuniamini
na kuweza kunipa kazi za Chuo kufanya…mimi naiona VETA kama mzazi,"amesema
"VETA
haimuachi mtu wakati wote wanakufuatilia na kama kuna mahali wanaona wanaweza
kukusaidia basi wanakupa kipaumbele cha kwanza. Pia wana utaratibu mzuri wa
kumfuatilia mwanafunzi wao aliyehitimu masomo katika VETA popote alipo na
wanakua na taarifa zao na kuendelea kuwasaidia," ameongeza.
Irene amewashauri watanzania wote hususani wazazi
kuona uwepo wa vyuo vya VETA nchini kuwa fursa kubwa ya ukombozi wa fikra za
vijana kiuchumi katika mapambano ya kujikomboa na ukosefu wa ajira ambapo
amesema kuwa kiwango bora cha elimu kinachotolewa na VETA kitapelekea kujiajiri
wenyewe na kuweza kuendesha maisha yao mahala popote ndani na nje ya Tanzania.



No comments:
Post a Comment