Walimu 16 wa ufundi stadi kwenye vyuo vya Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wamepatiwa mafunzo juu utekelezaji wa miongozo
ya kuboresha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa watu wenye mahitaji
maalum nchini.
Akifungua warsha kwa walimu hao katika chuo cha VETA Dodoma leo tarehe 6 Februari, 2023, Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa VETA, Ndg. Abdallah Ngodu, amesema miongozo hiyo inalenga kuweka mazingira wezeshi ya kujifunzia na kufundishia watu wenye mahitaji maalum wanaojiunga na mafunzo mbalimbali kwenye vyuo vya VETA.
Amesema idadi ya watu wenye mahitaji maalum wanaojiunga na vyuo vya VETA nchini inaendelea kuongezeka siku hadi siku na kwamba VETA imeona umuhimu wa kutoa kipaumbele kwenye kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa elimu ya ufundi stadi na kuhakikisha walimu wanaelewa vyema mbinu za ufundishaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Kwa mujibu wa Ndg. Ngodu, VETA iliandaa miongozo miwili
ambapo mwongozo wa kwanza unaelekeza namna ya kuwajumuisha watu wenye mahitaji
maalum kwenye mafunzo kuanzia hatua ya kuwatambua hadi kuwaingiza kwenye kozi
na mwongozo wa pili unaainisha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji ambao walimu
watautumia kuwafundisha watu hao bila kuwabagua.
“Tunatoa mafunzo kwa walimu ili waweze kuielewa vyema
miongozo hii na kuitumia kutoa mafunzo na kuhakikisha watu wenye mahitaji
maalum wenye kuhitaji mafunzo ya ufundi stadi kwenye vyuo vyetu wanayapata kwa
ufanisi ili yawasaidie kwenye maisha yao,” amesema
Afisa Mkuza Mitaala wa VETA, Bi .Happiness Salema,
amesema msisitizo uliowekwa katika miongozo hiyo ni kuwajumuisha watu wenye
mahitaji maalum kupata mafunzo pamoja na wasiokuwa na mahitaji maalum na kuweka
miundombinu ya kuwawezesha watu hao kujifunza bila vikwazo.
Naye Mkufunzi Mwandamizi wa Chuo cha Ualimu wa Ufundi
Stadi Morogoro, Ndg. Rodgers Sabuni, amesema kupitia miongozo hiyo walimu wa
vyuo vya VETA wataweza kuwahudumia vizuri zaidi wanafunzi wenye mahitaji maalum
tofauti na walivyokuwa wakifanya awali ambapo wengi wao walitumia uzoefu.
Mwalimu wa fani ya Useremala katika Chuo cha VETA Dar es
Salaam, Ndg. Salehe Omari amesema mafunzo yaliyoanza kutolewa yamempa fursa ya
kufahamu zaidi kwa utaalamu namna ya kuhudumia watu wenye mahitaji maalum na
kwamba miongozo iliyoandaliwa itasaidia kuongeza idadi ya walimu wengi zaidi wa
kutoa mafunzo hayo.
Naye mwalimu wa Fani ya Mapishi katika Chuo cha VETA
Mbeya, Ndg. Asibatike William amesema kupitia mwongozo huo VETA itaweza kuweka
mazingira rafiki zaidi ya kufundishia watu wenye mahitaji maalum na kuwajengea
ari walimu ya kujiamini zaidi katika kuhudumia wanafunzi hao.
Warsha ya kuwajengea uwezo walimu wa VETA juu ya mbinu za
ufundishaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum awamu ya kwanza inajumuisha
walimu kutoka katika vyuo vya VETA wa
fani za Useremala, Uungaji na Uchomeleaji Vyuma, Ushonaji, Ufundi Umeme,
TEHAMA, Mapishi na Utengenezaji wa Bidhaa za Ngozi. Warsha hiyo inafanyika kwa
siku tatu kuanzia tarehe 6 hadi 8 Februari, 2023.




No comments:
Post a Comment