CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Thursday 22 February 2018

Wahitimu 159 wa Ufundi Stadi Wilaya ya Temeke wapatiwa vitendea kazi


Jumla ya vijana 159 wa wilaya ya Temeke jijini dar es Salaam waliohitimu mafunzo ya ufundi stadi   wamepatiwa vifaa vya kufanyia kazi vyenye thamani ya shilingi milioni 33.

Vijana hao waliohitimu katika mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) wamepatiwa vifaa hivyo kupitia vikundi vyao walivyoviunda na kuvisajili rasmi.
Akikabidhi vifaa hivyo  katika hafla fupi iliyofanyika katika Chuo cha VETA Dar es Salaam tarehe 20 February , 2018 mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam  Fortunatus Kagoro  alisema  anaamini kupitia uwezeshwaji huo vijana hao wataweza kuboresha shughuli zao na kujiingizia kipato.
Alisema  changamoto kubwa kwa vijana kwa sasa ni ukosefu wa ajira na kuhamasisha vijana kutumia fursa zinazojitokeza za kujipatia ujuzi kupitia vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa kuwa kijana akishapata ujuzi ni rahisi kupata ajira kwa kuajiriwa au kujiajiri.

Bwana Kagoro aliwashukuru na kuwapa pongezi wadau walioshiriki kufanikisha mradi huo mpaka kufikia hapo na kuwataka wadau hao kufikiria namna ya kuwafikia vijana wengi zaidi nchini.

Aliwataka vijana kutumia vifaa hivyo walivyovipata kuboresha shughuli zao za kiufundi kulingana na fani walizosoma, hivyo kujiletea maendeleo binafsi, kwa familia zao na jamii kwa ujumla.
Akitoa taarifa ya mradi,Mkuu wa chuo cha VETA Dar es salaam  Douglas Kipokola alisema Vijana wapatao 2314 wamekwishanufaika na mafunzo katika awamu sitakati yao vijana 1,872 wameshahitimu mafunzo na wengine 486 bado wanaendelea na mafunzo ya nadharia na vitendo.
“Vijana hawa wamepatiwa mafunzo katika fani za udereva, mapishi na mapambo, ushonaji, Uungaji Vyuma, ufundi magari, umeme wa Magari na Umeme wa Majumbani” Alisema.

Aliwahamasisha vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi stadi kuunda vikundi vya uzalishaji mali kwani ni rahisi kuwawezesha vijana wakiwa katika vikundi huku akitoa taarifa kuwa   jumla ya vikundi 26 vilipatiwa vifaa katika awamu ya kwanza ya mradi na vikundi 50 vimepatiwa vifaa hivyo kwa awamu ya pili katika  wilaya za Ilala na Temeke.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Plan International  Adam Mambea  alisema lengo la mradi lilikuwa kufikia vijana wapatao 9,100  lakini kutokana kuongezeka kwa mahitaji na mwitikio kuwa mkubwa wameona waongeze vijana wengine 1002 ili kufikia idadi ya vijana 10,000 katika wilaya za Ilala na Temeke .

Meneja Mradi wa Plan International Saimon Ndembeka alisema lengo kubwa la mradi huo ni kuwakomboa vijana wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapatia mafunzo ya ufundi stadi.

Alisema katika awamu ya kwanza walifanikiwa kutoa vifaa vya zaidi ya shilingi milioni 40 na sasa wametoa vifaa vya zaidi ya shilingi milioni 33 kwa ajili ya vijana hao.
Mradi huo unafadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya na kutekelezwa na shirika la  Plan International Tanzania kwa kushirikiana na  Mamlaka ya Mafunzo ya ufundi stadi ( VETA ), shirika la VSO, CODERT na UHIKI na CCBRT
 Mradi huo ulipangwa kufanyika kwa  miaka mitatu (2015 hadi 2018)   na unatekelezwa  katika mikoa mitano ambayo ni Dar es salaam, Pwani, Morogoro, Lindi na Mtwara ukihusisha vyuo vya  VETA DSM (Chang’ombe), VETA Lindi, VETA Pwani, VETA Mikumi na VETA Mtwara
Mradi huu ulizinduliwa rasmi mwezi Septemba mwaka 2015 na aliyekua Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dr. Mohammed Gharib Bilal.




No comments:

Post a Comment