CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Monday 12 February 2018

VETA yakutanisha wadau kujadili mpango mkakati wa miaka mitano


Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)  imeandaa mkutano wa wadau kwa lengo la kuwasilisha mpango mkakati wake wa miaka mitano na kupokea maoni yao.

Akifungua warsha hiyo Dar es Salaam kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi  Bw Peter Maduki leo tarehe 12/02/2018, Mjumbe wa Bodi hiyo Bw Suleiman Lolila alisema kuwa mpango mkakati huo unatoa picha halisi ya nini mamlaka hiyo (VETA) inatarajia kufanya ndani ya miaka mitano.

Alitaja malengo makuu ya mkakati huo kuwa ni kuboresha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi , kupanua wigo wa utoaji mafunzo ya elimu na ufundi stadi ili kufikia makundi mengi zaidi na kuimarisha menejimenti ya VETA .

Malengo mengine ni kupunguza maambukizi wa virusi vya ukimwi na kuboresha huduma saidizi na kutekeleza mpango wa taifa dhidi ya rushwa.

Aliwataka wadau hao kutoa mawazo yao ili kuboresha mpango mkakati huo na kwamba Bodi hiyo itapokea mawazo hayo na kuyajumuisha katika mpango mkakati na kusimamia utekelezaji wake kwa kuweka mazingira rafiki na kutoa usimamizi wa karibu kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Bwire Ndazi amesema kuwa Mpango mkakakati huo umeandaliwa kwa kuzingatia hali halisi ya kiuchumi na kijamii ili kuhakikisha ajenda ya serikali ya kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda inafikiwa.

“Katika miaka mitano ijayo (2018/2019 hadi 2022/2023) mamlaka hiyo imejikita katika kuhakikisha uboreshaji wa utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kuwa na mafundi stadi mahiri na wa kutosha nchini.
  
Baadhi ya malengo ni 


Kuongeza udahili wa wanafunzi katika vyuo vya ufundi stadi kutoka 200,000 hadi 700,000



Udahili wa watu 400 wenye mahitaji maalum kila mwaka



Udahili wa vijana 2400 wanaotoka katika mazingira magumu kila mwaka

Kuongeza udahili wa wanafunzi wa kike kutoka asilimia 35 hadi 45



Utambuzi na Urasimishaji wa vijana 200,000 waliopata mafunzo kupitia mfumo usio rasmi

Mkutano huo umehusisha wadau mbalimbali wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi ikiwemo maafisa wa serikali, wawakilishi kutoka mashirika ya kimataifa kama ILO, ISTEP, IYF na VSO, wawakilishi kutoka katika viwanda, watoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na wazazi.

 


No comments:

Post a Comment