Ujenzi wa vyuo na karakana za mafunzo maeneo
mbalimbali nchini
Ukarabati vyuo na uboreshaji karakana za mafunzo
Ni Miaka
miwili imetimia tangu serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mh. Rais Dkt John Pombe
Magufuli, iingie madarakani. Msisitizo na mwelekeo wa Mh. Rais na serikali yake, kama yalivyo malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 na azma ya Mpango
wa II wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17-2020/21, ni kuifanya
Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaotegemezwa na viwanda. Miongoni mwa
mikakati muhimu ni kuhakikisha kunakuwepo nguvukazi ya kutosha na yenye uwezo
wa kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kufikia malengo hayo ya
kitaifa.
Hivyo
kuwa na nguvukazi yenye ujuzi ni suala muhimu mno na lisiloepukika, kwani ndilo
huchangia kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha shughuli za uzalishaji na
uendeshaji wa viwanda zinafanyika kwa ufanisi na kwa tija. Vilevile, ujuzi utawawezesha
wananchi kuingia katika sekta rasmi ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kujiajiri
kwa kuanzisha viwanda vidogovidogo katika vikundi au wakiwa mmoja mmoja.
Umuhimu zaidi na wa kipekee ni kwa kundi lenye ujuzi wa ufundi stadi, kwani
hili ndo kundi kubwa linalohitajika katika kuendesha shughuli viwandani. Hapa ndipo
jukumu la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
linapojidhihirisha.
VETA
ikiwa ndio yenye dhamana ya kuandaa mafundi stadi, inatambua kuwa katika kipindi hiki kunahitajika
mikakati thabiti ya kupanua wigo na kuimarisha ubora wa mafunzo ili kwenda
sambamba na mahitaji ya kuanzisha na kuendeleza viwanda.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Bwire Ndazi anabainisha mikakati mbalimbali
ambayo VETA inaendelea kuipanga na kuitekeleza ili kuendelea kuongeza
uzalishaji wa nguvukazi yenye ujuzi katika ufundi stadi.
“Matamanio
yetu ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania mwenye fursa kuhitaji fursa ya elimu na
mafunzo ya ufundi stadi nchini anaipata katika ubora unaohitajika ili kujenga
nguvukazi yenye ujuzi na umahiri itakayoiwezesha nchi kufikia azma ya Mpango wa
II wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP II) kujenga chumi wa viwanda,” Dkt. Ndazi
anafafanua.
Anaeleza
kuwa, moja ya maeneo muhimu yanayotiliwa mkazo na VETA ni kuendelea kujenga,
kukarabati na kuimarisha vyuo na karakana za mafunzo katika maeneo mbalimbali
ili vijana na wananchi wengi kwa ujumla waweze kupata fursa za mafunzo kwa
urahisi. Mataraji ni kuongeza vyuo vinavyomilikiwa na VETA kutoka 28 mwaka 2015 hadi41
kufikia mwaka 2019. Vilevile, kujenga karakana na kuboresha zilizopo,
pamoja na kukarabati vyuo vilivyopo.
“Hadi
sasa, kuna mipango ya miradi zaidi ya ishirini inayohusisha ujenzi, ukarabati
na uboreshaji na uimarishaji wa karakana za mafunzo,” anasema Dkt. Ndazi.
Anaitaja
baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa vyuo vya mikoa vinne (4), katika mikoa ya
Rukwa, Geita, Simiyu na Njombe, miradi ambayo iko katika hatua mbalimbali. Vilevile
ujenzi
wa vyuo vipya sita (6) katika wilaya za Ukerewe, Nyasa, Namtumbo, Kilindi,
Chunya, na Chato na ukarabati vyuo viwili (2) vya wilaya za Karagwe na Korogwe pia
uko katika hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujezi wa misingi, kuta,
uezekaji, utoaji zabuni na uingiaji mikataba.
Dkt. Ndazi anataja baadhi
ya mafanikio ya hivi karibuni katika juhudi za ujenzi na ukarabati wa vyuo kuwa
ni pamoja na kukamilisha ukarabati wa chuo cha Ufundi Stadi Busokelo, Mkoani
Mbeya kilichhoanza kutoa mafunzo Machi, 2017 katika fani za umeme, useramala na
ushonaji. Vilevile, VETA ilikarabati Chuo cha Ufundi stadi Nkowe, wilaya ya
Ruangwa, mkoani Lindi na kukiwezesha chuo kuendeleza mafunzo katika mazingira
bora zaidi.
“Katika
kuzidi kuimarisha na kuboresha mafunzo ya vitendo, ambayo ndiyo nguzo kuu ya
ufundi stadi, suala la uboreshaji wa karakana nalo tunalipa kipaumbele
kikubwa,” anaeleza Dkt. Ndazi na kuongeza, “tunajenga karakana na kununua vifaa
mbalimbali vya mafunzo ili viweze kutumiwa na walimu na wanafunzi katika masomo
ya vitendo.”
Anazitaja
juhudi za uboreshaji na uimarishaji wa karakana kuwa ni pamoja na ujenzi wa
Karakana ya kisasa ya Useremala katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi Dodoma
(VETA Dodoma) ambayo imekamilika kwa
zaidi ya asilimia 90; Ujenzi wa karakana za Useremala na umeme wa Magari Chuo
cha Mkoa Morogoro-Kihonda ambao uko katika hatua ya ukamilishaji; na ujenzi wa
Karakana ya Umeme wa Viwandani katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa-VETA Mwanza
ambao uko katika hatua ya kuezeka.
Anaongeza
kuwa, Mamlaka inasambaza
vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika Vyuo vya Ufundi Stadi vya
Kihonda-Morogoro, Oljoro-Arusha, Kasulu-Kigoma, Mbeya na Chuo cha Walimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC)
na inatarajia kufanya hivyo pia katika vyuo vya Singida na Iringa na kwenye
karakana ya Useremala ya Chuo cha VETA Dodoma.
Dkt. Ndazi anaeleza
kuwa VETA inatambua kuwa ujenzi wa vyuo, karakana na uwekaji wa vifaa vya
kufundishia na kujifunzia ni wa gharama kubwa na hivyo ni vigumu kumudu kujenga
vyuo vingi katika maeneo mbalimbali kwa muda mfupi. Kwa hiyo, ili kukabiliana
na mahitaji makubwa ya mafunzo, Mamlaka inabuni mbinu na mifumo mingine za
kupanua fursa za mafunzo ya ufundi stadi sambamba na ujenzi wa vyuo.
Miongoni mwa mbinu
hizo ni pamoja na kuimarisha mfumo wa mafunzo ya nje ya chuo kwa Chuo cha
Walimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC); utoaji wa kozi fupifupi za ufundi
stadi; kuhamasisha na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika kuwekeza
katika utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa kukaribisha ushirikiano pamoja na kutumia teknolojia ya habari na
mawasiliano (TEHAMA) kama vile mitandao ya simu kutoa mafunzo. Pia kutekeleza
mwongozo wa Kitaifa wa Uwanagenzi (Apprenticeship) kwa kupanua utoaji wa
mafunzo yanayohusisha chuo na mahala pa kazi kutoka katika chuo cha Moshi, Dar
es Salaam na Mwanza hadi nchi nzima.
No comments:
Post a Comment