CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Friday 23 March 2018

Ufanisi wa sekta isiyo rasmi kuimarika kupitia mafunzo ya ufundi stadi


Mikakati na mwelekeo wa serikali sasa ni kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati na zaidi uchumi unaoendeshwa na viwanda. Wakati tukikwa katika mwelekeo huo wa kiuchumi, moja ya mambo muhimu ya kutambua kuwepo kwa kundi kubwa  nchini linaloendesha shughuli zao za kiuchumi katika sekta isiyo rasmi ambapo shughuli zao aghalabu hutawaliwa na mazingira duni, ujuzi hafifu na tija ndogo. Kwa kutambua hilo, ni vyema kuweka mikakati ya kuwezesha kundi hili lenye wananchi wengi kuboresha shughuli zao na hivyo kukua kiuchumi sambamba na mwelekeo wa nchi.

“Moja ya wajibu muhimu katika kusaidia sekta isiyo rasmi ni kuboresha ujuzi na maarifa yao,” anasema Dkt. Bwire Ndazi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Katika mahojiano maalum na mwandishi wa makala hii, Dkt. Ndazi alieleza kuwa umuhimu na mchango wa sekta isiyo rasmi katika kukabiliana na tatizo la ajira, kuongeza kipato kwa watu mmoja mmoja na kuchangia katika uchumi wa nchi kwa ujumla,VETA imebuni programu mbalimbali kwa ajili ya kusaidia kuboresha ujuzi na maarifa, hivyo kuongeza tija na ubora wa bidhaa na huduma katika sekta isiyo rasmi.

“Kwa sasa, VETA inatekeleza programu mbili zinazolenga kuboresha ujuzi katika sekta isiyo rasmi, ambazo ni Mpango Jumuishi wa Mafunzo ya Kukuza Ujasiriamali katika sekta isiyo rasmi na Utambuzi na Urasimishaji wa Ujuzi uliopatikana nje ya Mfumo Rasmi,” anafafanua.
Akizungumzia juu ya Mpango Jumuishi wa Mafunzo ya Kukuza Ujasiriamali katika sekta isiyo rasmi Dkt, Ndazi anaeleza kuwa pango huo unalenga zaidi katika kupanua fursa za kujiajiri, kuongeza tija na ubora wa  bidhaa na huduma kwenye sekta isiyo rasmi kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi.  Mpango huo umeweka mfumo maalum wa kufanya tathmini ya hali ya kiuchumi na kijamii katika mazingira husika, ikiwemo matarajio ya kundi la walengwa. Nia hasa ni kukuza ujasiriamali ili kuhakikisha kuwa matokeo ya biashara zao yanakuwa ni yenye tija na kuongeza ajira.  Pamoja na kukuza ujasiriamali, mpango huu unalenga katika kuhamasisha usawa wa kijinsia na ushiriki wa vijana katika ujasiriamali na kujipatia kipato.

Miongoni mwa manufaa ya mpango huo kama alivyoyafafanua Dkt Ndzi ni kuunganisha shughuli za kiuchumi na kijamii nchini na elimu na mafunzo ya ufundi stadi; kuongeaza stadi za ujasiriamali na maisha katika mafunzo; na mafunzo kuzingatia mahitaji ya jamii husika;

Aliyataja mafanikio ya mpango huo kuwa katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2016 zaidi ya wajasiriamali 6500 walinufaika na mpango huu, wakiwemo wanawake na vijana katika maeneo mbalimbali nchini.

Kundi lingine katika mfumo usio rasmi ni mafundi mbalimbali wanaoendesha shughuli zao na kutoa huduma mbalimbali katika jamii, lakini ujuzi wao wameupata pasipo kupitia mafunzo rasmi ya chuoni. Kwa lugha nyingine, ujuzi wao wameupatia mahala pa kazi pekee.

Katika kusaidia kundi hili, Dkt Ndazi anaeleza kuwa VETA imebuni mpango wa Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi Uliopatikana nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo (Recognition of Prior Learning). Mpango huu unalenga katika kutambua, kutathmini, kutoa mafunzo ya kuziba upungufu wa ujuzi kwa wanagenzi katika fani husika, kisha kutunuku vyeti ujuzi wa mafundi (wanagenzi) uliopatikana kupitia mfumo usio rasmi.

Nia hasa ni kuwasaidia wanagenzi kupata kazi zenye staha; kupandishwa madaraja katika ajira; kukidhi sifa za kujiendeleza katika taaluma zao; kuwajengea uwezo wa kushiriki na kushindana kikamilifu katika soko la ajira; kuinua tija mahali pa kazi na kusaidia waajiri au wenye makampuni kukidhi viwango katika eneo la rasilimali watu.

“Hivyo, kitendo cha kuwafikia walengwa hawa (wanagenzi) kinatoa fursa ya kipekee kwani matumaini ya kufikia  ndoto zao, yatapata msukumo mkubwa. Ni zoezi ambalo pia linakwenda sambamba na lengo la kuandaa nguvu kazi kwa ajili ya uchumi wa viwanda na Licha ya kuongeza ushiriki wa vijana katika kukuza uchumi wao na kuwa na mchango zaidi katika uchumi wa Taifa,” anaongeza.

Anafafanua kuwa mpango huu ulianza tangu mwaka 2009, ingawa ulianza kwa majaribio. Katika kipindi hicho cha majaribio wanagenzi wapatao 570 walitambuliwa, 487 walifanyiwa tathmini na 400 walifaulu na kutunukiwa vyeti. Zoezi hili lilifanyika katika mikoa sita (6) ya Mtwara, Lindi, Morogoro, Mwanza, Mbeya na  Dar es Salaam.
Mpango huu ulizinduliwa rasmi mwaka 2014 na uliendelea kutekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Kazi Duniani (ILO) na wadau wengine na hadi kufikia  Oktoba 2016, jumla ya wanagenzi 1,824 wakiwemo wanawake 197 na waume 1,627 walikuwa wametambuliwa. Kati ya hao wanawake 148, na wanaume 1,145 walifanyiwa tathmini ya ujuzi wao na 1,103 walifaulu zoezi la tathmini na hivyo kutunukiwa vyeti.

Januari 2017, VETA iliungwa mkono na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi,  Vijana, Ajira, na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana kuendeleza mpango huu na imekusudia kurasimisha ujuzi wa mafundi wasiopungua 3,900 nchini kote katika fani za Ufundi Magari, Useremala, Uashi (ujenzi), Upishi na Uhudumu wa Hoteli na baa.
Kwa mujibu wa Dkt Ndazi jumla ya wanagenzi 22,367 walijitokeza kufanyiwa tathimini ya ujuzi wao wakiwemo wanawake 2,320 (sawa na na wanaume 20,047 ambapo jumla ya wanagenzi 14,424 walikidhi vigezo vya kufanyiwa tathmini. Ufinyu wa bajeti ndio hasa uliofanya idadi ya wanagenzi watakaofanyiwa tathmini kuishia 3900 ingawa wote waliokidhi vigezo wataendelea kuwekwa katika orodha ya ziada na pindi hali ya kifedha ikiruhusu watafanyiwa pia tathmini.

Mrejesho wa kutoka kwa wanagenzi waliofikiwa na mpango huu  ni kuwa wengi wao waliweza kujiamini zaidi katika kazi zao; wengine waliajiriwa; wengine walipata zabuni za kazi serikalin na wengine waliongezewa mishahara.

Dkt Ndazi anasema matarajio ni kuwa ni kuongeza wigo wa wanagenzi wanaofanyiwa tathmini ya ujuzi na kujumuisha nyanja nyingine kama Ushonaji, Ufundi bomba, Uungaji vyuma (Welding and Metal fabrication), urekebishaji wa bodi za magari (Auto body repair) na fani nyingine ambazo hazikuweza kufikiwa hapo awali.
Sambamba na mipango hiyo, Dkt Ndazi anaongeza kuwa VETA imekuwa ikitazama pia mambo ya kiuchumi ikiwemo miradi mikubwa inayojitokeza katika jamii na kuandaa mipango ya kuwezesha wananchi waliopo katika sekta isiyo rasmi. Mathalani, katika Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania, VETA imefanya tathmini na kubaini fursa mbalimbali ambazo wananchi wanaweza kunufaika nazo katika mradi huo. Imeweza kutambua na kuainisha pia mambo ya kiujuzi yanayohitajika kuboreshwa katika sekta isiyo rasmi ili kuweza kutoa huduma bora katika mahitaji ambayo yatachochewa na ujenzi wa bomba hilo. Miongoni mwa ujuzi unaoweza kuboreshwa, hivyo kuwasaidia walio katika sekta isiyo rasmi kunufaika na ujenzi wa bomba la mafuta ni stadi za ufugaji, kilimo cha bustani, usagishaji, usindikaji, ufungashaji na uhifadhi wa mazao pamoja na uandaaji wa nyama. Kwa sasa mamlaka inaandaa mpango wa mafunzo ya muda mfupi kwa ajili ya jamii zilizopo katika wilaya mbalimbali ambamo bomba la mafuta litapita.

No comments:

Post a Comment