Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, William Ole Nasha amewataka vijana na umma wa Watanzania kwa ujumla
kutambua umuhimu na kutumia fursa za mafunzo ya ufundi stadi, kwani fani hizo
sasa zinahitajika zaidi nchini, hivyo hata wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu
sasa wanakimbilia kujifunza ufundi stadi.
Akiongea baada ya kutembelea chuo cha
VETA Manyara, Jumatatu, tarehe 8 Octoba, 2018, Ole Nasha alisema sasa kuna
msukumo mkubwa wa elimu ya ufundi kuliko wakati mwingine wowote kutokana na
mwelekeo wa kiuchumi pamoja na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii nchini.
Alizitaka sababu mahsusi zinazoipa
umuhimu mkubwa elimu ya ufundi kuwa ni pamoja uhitaji wa nguvu kazi ya ufundi
kwenye uchumi wa viwanda na uwekezaji mkubwa wa serikali kwenye ujenzi wa
miundombinu mbalimbali.
“Viwanda viko vingi, vidogo, vya kati
na vikubwa lakini vyote vina sifa moja, vinahitaji nguvukazi mahiri ya ufundi. Lakini
sote ni mashahidi kuhusu uwekezaji wa serikali kwenye miundombinu, ikiwemo
ujenze wa reli ya kisasa ya kutumia umeme (standard gauge). Uwekezaji wa
miundombinu kama ile hauwezi ukaenda bila ya mafundi. Uuwekezaji ambao
unahitaji mafundi si kwa ajili ya ujenzi pekee bali hata katika matengenezo
mengine baada ya kukamilika kwake,” alisema.
Alitoa mfano mwingine wa uwekezaji
mkubwa unaohitaji mafundi ni ule wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima
nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania ambalo ujenzi wake
unatarajiwa kutoa fursa nyingi kwa mafundi.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni
urahisi mkubwa kwa wahitimu wa ufundi kupata ajira, kwa kuwa na fursa kubwa za
kuajiriwa au kujiajiri, huku akiwataka wanafunzi wa VETA kujiona wamechagua
njia sahihi na yenye manufaa makubwa kwao.
“Kwa hiyo kwanza jiondoeni unyonge
kwamba mimi nasoma VETA tu, lakini mwenzangu kaenda chuo kikuu. Kwa taarifa
yenu, mna nafasi kubwa ya ajira kuliko mtu ambaye ameenda chuo kikuu. Miaka ya
karibuni tumeanza kuona wimbi kubwa la wanafunzi waliomaliza chuo kikuu wakija
kuomba kujiunga VETA. Mimi nimekutana nao wengi, ukimuuliza anasema nimekwenda
kujifunza nadharia lakini sijaona kitu ilichonisaidia. Ninyi mnafahamu nadharia
na vitendo,” alifafanua.
Katika hafla hiyo baadhi ya wanafunzi
wa VETA Manyara waliiomba serikali kuweka utaratibu wa kuwasaidia wahitimu wa
ufundi stadi kupata vifaa ili waweze kujiajiri, huku mwanafunzi Matheo Masoye
wa mwaka wa pili fani ya Umeme akiiomba serikali kuandaa mazingira mazuri kwa
watu wenye ulemavu nao kupata elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili pia
wajikwamue kiuchumi.
Akijibu hizo Ole Nasha aliitaka VETA
kuhakikisha kuna mazingira ya kuwawezesha wenye ulemavu nao kupata fursa za
mafunzo ya ufundi stadi kama ilivyo kwa watu wengine.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa
VETA, Dkt Pancras Bujulu alishauri kuanzisha mfuko maalum (revolving fund)
katika halmashauri kwa ajili ya kuwasaidia wahitimu wa ufundi stadi vifaa na
mahitaji mengine ya kuwawezesha kujiajiri.
“kwa sababu shughuli hizo zinazalisha,
wapewe utaratibu wa kulipa ili na wengine wanufaike,” alisema.
Katika ziara hiyo, Naibu
Waziri aliambatana viongozi na maafisa wengine wa wilaya ya Babati akiwemo Mkuu
wa Wilaya ya Babati, Elizabeth Simon Kitundu, Mbunge wa Babati Mjini, Pauline
Gekul na Mbunge wa Babati Vijijini Virajlal Jituson na alikutana
pia na Wajumbe wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi pamoja na
Menejimenti na wafanyakazi wa VETA kutoka Makao Makuu, VETA Kanda ya Kaskazini
na Chuo cha VETA Manyara.
No comments:
Post a Comment