- Ujenzi wa vyuo vya Geita, Rukwa na Chato waanza
- Yadhamiria kufika kila mkoa
Mwenyekiti wa Bodi ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Peter Maduki anataja baadhi ya miradi hiyo
kuwa ni pamoja na ujenzi wa vyuo vya mikoa vinne katika mikoa ya Geita, Rukwa,
Simiyu na Njombe inayotegemewa kumaliza na kuanza kutoa mafunzo mwaka 2019.
Anasema vyuo vingine
vinavyotegemewa kujengwa ni vya wilaya sita za Ukerewe, Nyasa, Namtumbo,
Kilindi, Chunya, na Chato na ukarabati wa vyuo viwili vya wilaya za Karagwe na
Korogwe ambapo michakato yake ipo katika hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na
ujenzi wa misingi, kuta,uezekaji, utoaji zabuni na uingiaji mikataba.
Kwa mujibu wa Maduki, ujenzi wa vyuo hivyo kwa mikoa na wilaya una
lengo la kutekeleza Mpango wa Kimkakati wa VETA namba tano (VETA
Corporate Plan V) ambao unatekelezwa kuanzia mwaka 2018/2019 hadi
2022/2023 ambapo pamoja na mambo mengine unalenga kuongeza udahili wa wanafunzi
katika vyuo vya ufundi stadi kutoka 200,000 hivi sasa hadi kufikia 700,000 ifikapo
mwaka 2020.
Maduki anaongeza kuwa jitihada hizo zinaenda sanjari na
utekelezaji wa nia njema ya Serikali ya awamu ya tano ya kuhakikisha kuwa
vijana wanapata ujuzi stahiki utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri ili
kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi na kuhakikisha nchi inafikia uchumi
wa kati ifikapo 2025.
Kwa sasa VETA inamiliki vyuo 28 vya ufundi stadi katika mikoa
mbalimbali nchini na chuo kimoja cha kutoa mafunzo ya ualimu wa ufundi stadi
kilichoko mkoani Morogoro huku ikisimamia utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi
katika vyuo 566 ilivyovisajili vinavyomilikiwa na watu binafsi, mashirika ya
dini, taasisi za serikali naasasi za kiraia. Vyuo hivi vinatoa mafunzo
katika fani zaidi ya 80 zilivyogawanywa katika sekta za fani 13 ambazo ni
ufundi mitambo; ufundi umeme; ufundi ujenzi; ufundi magari; huduma za biashara;
mavazi na nguo. Sekta nyingine ni usafirishaji na uchukuzi; uziduaji
(utafutaji, uchimbaji na uchakataji madini); uchapaji; urembo, ususi na
umaridadi; kilimo na usindikaji chakula; hoteli na utalii pamoja na sanaa za
mikono na maonesho.
Mwezi Agosti, 2018 VETA ilikabidhi maeneo ya ujenzi wa vyuo viwili
vya Mikoa ya Geita na Rukwa na chuo cha Wilaya ya Chato kwa wakandarasi kwa
ajili ya kuanza ujenzi unaotarajiwa kumalizika ndani ya miezi 12 baada ya
makabidhiano hayo.
Tarehe 6 na 7 Agosti, 2018 makabidhiano ya miradi ya ujenzi wa vyuo
vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi
(VETA) vya mkoa wa Geita na Wilaya ya Chato yalifanyika na kushuhudiwa na Mkuu
wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel pamoja na viongozi wa wilaya ya Chato.
Akikabidhi rasmi nyaraka za ujenzi wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi (VETA) cha Mkoa wa Geita chenye ukubwa wa hekta 27 kwa Mkandarasi
anayejenga chuo hicho Kampuni ya Kitanzania Skywards Construction,
Mwenyekiti wa Bodi ya VETA Peter Maduki alisema kuwa gharama ya
ujenzi wa chuo hicho ni Sh bilioni 9.9 fedha za mkopo kutoka benki ya Maendeleo
ya Afrika (AfDB). Kwa upande wa chuo cha wilaya ya Chato chenye ukubwa wa ekari
70, Maduki alisema ujenzi wake utagharimu kiasi cha Sh bilioni 10.7 ambazo ni fedha za ndani ambapo ujenzi wa
chuo hicho unafanywa na kampuni ya Kitanzania ya C.F Builders yenye makao yake
jijini Mwanza.
Maduki alisema vyuo hivyo viwili vitakapokamilika
vitakuwa na uwezo wa kudahili jumla ya wanafunzi 2940, ambapo kwa chuo cha mkoa
wa Geita pekee kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 660 kwa ngazi
tatu kwa mafunzo ya muda mrefu kwa mwaka na wanafunzi wasiopungua 1000 kwa
mafunzo ya muda mfupi wakati Chuo cha VETA Chato kitakuwa na uwezo wa
kudahili wanafunzi 480 kwa ngazi hizo tatu
za mafunzo ya muda mrefu na wanafunzi wasiopungua 800 kwa mafunzo ya muda
mfupi. Alizitaja baadhi ya fani zitakazotolewa katika
vyuo hivyo kuwa ni pamoja na Ufundi wa Mitambo Mizito; Ufundi Elektroniki;
Mechatronics; Ufundi Umeme wa Magari; Ufundi Uashi; Ufundi Umeme; Ufundi bomba; Ukarimu na Usindikaji wa Samaki;
Useremala; Mafunzo ya Uhazili na
Compyuta na Ufundi wa vifaa tiba.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel alimshukuru Rais John
Magufuli kwa kazi kubwa anayofanya ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini
sambamba na ujenzi wa vyuo hivyo vya kisasa ambavyo vitawawezesha wananchi hasa
vijana kupata ujuzi ili waweze kujiajiri sanjari na kuwavutia wawekezaji kuwekeza
mkoani hapo. Alishauri uongozi wa VETA kutoa kipaumbele kwa fani zinazohusiana
na teknolojia ya uchimbaji ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kuchimba madini
kitaalam na kuongeza tija katika shughuli hiyo inayofanywa na vijana wengi
mkoani Geita. Aliwataka wakandarasi wa miradi hiyo kuhakikisha kuwa
wanakamilisha kazi ya ujenzi kwa muda uliopangwa kwa kuwa wananchi wa mkoa wa
Geita wana matarajio makubwa ya kuona miradi hiyo inakamilika kwa wakati
mwafaka na kwa ubora unaotarajiwa.
“Nitakuwa
nakagua ujenzi wa miradi hii mara kwa mara ili kuona utekelezaji wake…Nawasihi
sana wakandarasi wafanye kazi yao kama mikataba inavyoelekeza na kuzingatia
muda wa kukamilisha miradi hii”, alisema.
Kwa
upande wake Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Chato Elias Makori aliishukuru
serikali kwa kuamua kujenga chuo cha VETA wilayani Chato ambapo alisema
kitaongeza ajira, ujuzi kwa vijana sanjari na kupunguza umaskini.
Naye
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Batholomeo Manunga alisema ujio wa
mradi wa ujenzi wa chuo hicho utatatua changamoto ya ajira kwa vijana ambao
watapata ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa na kujiajiri na kukuza vipato vyao.
Ujenzi mwingine ni wa chuo cha VETA Mkoa wa Rukwa ambapo tarehe
30 Agosti, 2018 makabidhiano ya mradi wa ujenzi wa chuo hicho yalifanyika
wilayani Sumbawanga na kuhudhuriwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt Halfan Haule.
VETA ilikabidhi eneo la ujenzi kwa mkandarasi wa mradi huo, kampuni ya kichina
ya Tendar International Ltd. Ujenzi wa chuo hicho unatarajiwa kugharimu kiasi
cha Sh bilioni 10 fedha za mkopo kutoka benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na
umelenga kukidhi mahitaji ya ujuzi katika mkoa wa Rukwa na maeneo ya jirani.
Akizungumza
wakati wa makabidhiano ya mradi huo, Mwanasheria wa VETA Adelina Macha akimwakilisha
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA amesema dhamira ya VETA ni kujenga vyuo vya
ufundi stadi kila mkoa ili kuongeza udahili na uendelezaji ujuzi, hivyo kwenda
sambamba na kasi ya utekelezaji wa mkakati wa serikali kuelekea kwenye uchumi
wa viwanda, kwani VETA ina jukumu kubwa katika kuandaa nguvukazi kwa ajili ya
uchumi viwanda.
Kwa
mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Soko la Ajira, Mipango an Maendeleo wa VETA,
Hildergardis Bitegera,chuo hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili
wanafunzi 600 kwa mwaka kwa ngazi ya kwanza hadi ya tatu katika mafunzo ya muda
mrefu na wanafunzi wasiopungua 900 kwa mafunzo ya muda mfupi. Alisema kuwa
ujenzi huo utahusisha ujenzi wa karakana zitakazofundisha mafunzo kwa vitendo
katika fani za ufundi magari; uchomeleaji na uungaji vyuma; uhudumiaji na
uuzaji wa vinywaji; ufundi umeme; uandaaji na utayarishaji wa chakula; mafunzo
ya ukatibu muhtasi; ubunifu wa mavazi na ushonaji wa nguo; ufundi useremala;ufundi
uashi; ukarimu na utengenezaji wa chakula. Amesema utafiti wa soko la ajira
ulibaini kuwa shughuli kubwa za kiuchumi kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa ni
kilimo, ufugaji na uvuvi, hivyo miongoni mwa kozi zinazotarajiwa kufundishwa ni
usindikaji wa chakula ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Kaimu
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt Halfan Haule amesema kuwa Mkoa wa Rukwa ulikuwa na
uhitaji wa Chuo cha mafunzo ya Ufundi Stadi kwa muda mrefu, hivyo kuanza kwa ujenzi
huo kunaleta matumaini makubwa kwa vijana na wananchi wengine mkoani humo
kupata fursa za mafunzo ya ujuzi katika eneo lao huku akiishukuru serikali kwa
kuupa kipaumbele mkoa wa Rukwa na kuamua kujenga chuo hicho. Aliongeza kuwa
uwepo wa chuo hicho utahamasisha maendeleo na kuongeza kipato kwa wananchi wa
mkoa wa Rukwa ambapo ujuzi watakaopata utawawezesha kufanya usindikaji wa
chakula pamoja na uhifadhi wa mazao.
Kuhusu
ujenzi wa vyuo vya Mikoa ya Simiyu na Njombe, VETA inaendelea kukamilisha
taratibu za upatikanaji wa Wakandarasi na matarajio ni kwamba ujenzi wa vyuo
hivyo utaanza ndani ya mwaka huu 2018 ambapo zaidi ya Sh.bilioni 20
zinatarijiwa kutumika. Pamoja na ujenzi wa vyuo vipya, VETA inaendelea na
ukarabati wa vyuo vilivyopo ili kuboresha miundo mbinu na kuhakikisha mafunzo
yanayotolewa yanakidhi viwango vinavyotarajiwa hasa kwa kuendana na mahitaji ya
soko la ajira. Uboreshaji wa vyuo unahusisha ukarabati wa majengo ya zamani,
ujenzi wa karakana mpya pamoja na ujenzi wa mabweni kwa ajili ya wanafunzi.
Mnamo
Agosti 29, 2018 makabidhiano ya ujenzi wa mabweni mawili (kila jengo moja
likiwa na ghorofa moja) katika chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC)
yalifanyika kati ya VETA na kampuni ya Emirates Builders Co. Ltd ambapo zaidi
ya Sh. Bilioni 1 zitatumika kukamilisha ujenzi huo ndani ya miezi 12 ikiwa ni
mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB) kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi mbalimbali ya maendeleo katika kukuza sekta ya Elimu nchini. Kaimu Mkuu
wa Chuo hicho Habibu Bukko anasema ujenzi wa mabweni hayo ni mpango wa Serikali
ya awamu ya Tano unaolenga kuwezesha upatikanaji wa walimu wa kutosha wa ufundi
stadi nchini ili kuwezesha vijana wanaojiunga na vyuo vya ufundi stadi kupata
ujuzi stahiki wa kujiajiri na kuajiriwa. Anasema mabweni hayo yakikamilika
yatahudumia walimu wapatao 80 na hivyo kuongeza udahili wa walimu tarajali wa
bweni kutoka 142 kwa sasa hadi kufikia 222 ambapo idadi ya wanaume ni 144 na
wanawake ni 78.
Katika
chuo cha VETA Mwanza ujenzi wa karakana umeme wa viwandani umekamilika mwezi
Juni 2018 na karakana hiyo imeanza kutumika mwezi Julai ambapo wanafunzi 32 wa
fani hiyo wamesajiliwa.Ujenzi wa karakana hiyo uligharimu Shillingi Milioni 320
ambazo zilitolewa na serikali.
Uboreshaji miundombinu ya vyuo unaenda
sambamba na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kufundishia ambapo hivi karibuni vifaa
vinavyotumia teknolojia ya kisasa vya kufundishia vyenye thamani ya Euro
274,776, sawa na shilingi milioni 719 vimenunuliwa na vimeanza kutumika katika
chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC). Vifaa hivyo ni pamoja na viwakilishi
(Simulators) vya kufundishia fani ya Umeme wa Majumbani na Viwandani na vifaa
vya kufanyia mikutano na kutolea mafunzo kwa njia ya Video ambavyo kwa sasa
vinawezesha mikutano na mafunzo ya masafa kati ya Chuo cha MVTTC na Chuo cha
VETA cha Mkoa wa Dodoma pamoja na vifaa vilivyofungwa katika maabara ya lugha
(Language lab) ili kukuza uwezo wa wanafunzi kutumia lugha ya Kingereza na
Kifaransa.
Katika
chuo cha VETA Mtwara vifaa vya kufundishia vyenye thamani ya Dola za kimarekani
638,738, takriban shilingi Bil. 1.46 vimenunuliwa na vimeanza kusimikwa tayari
kwa matumizi.
Pamoja
na mkakati wa ujenzi wa vyuo vipya, VETA imekuwa ikibuni mbinu mbalimbali za
kupanua wigo wa utoaji mafunzo kwa kuwa mahitaji ya kupata ujuzi kwa
Watanzania, hususani vijana ni makubwa na yanazidi kuongezeka kila mara. Mfano
wa mbinu hizo ni utoaji wa mafunzo kwa njia mbalimbali za kisasa ikiwemo njia
ya mitandao ya simu na kompyuta, mfumo wa mafunzo kwa kushirikiana na viwanda/
makampuni (Uanagenzi Pacha), mafunzo ya muda mfupi katika sekta isiyo rasmi
pamoja na kufanya utambuzi na urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo
rasmi wa mafunzo.
VETA
ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 1 ya mwaka 1994 na kupewa dhamana ya kutoa,
kuratibu, kudhibiti, kugharimia na kuendeleza elimu na mafunzo ya ufundi stadi
nchini.
No comments:
Post a Comment