Serikali
za Tanzania na China zimetia saini makubaliano ya ujenzi wa Chuo cha Mkoa wa
Kagera utakaogharimu Shilingi za Kitanzania bilioni 22.4 zikiwa ni ufadhili
kutoka serikali ya China.
Makubaliano
hayo yametiwa saini leo tarehe 26 Novemba 2018 na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,
Sayansi na Taknolojia Dkt. Leonard Akwilapo aliyeiwakilisha Serikali ya
Tanzania na Yuan Lin, Mwakilishi Mkuu wa Uhusiano wa China na Tanzania katika
masuala ya Kiuchumi na Kibiashara aliyeiwakilisha Serikali ya Watu wa China.
Hafla
ya kutia saini makubaliano hayo ilifanyika katika ofisi za Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia Jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na wawakilishi
mbalimbali wa pande zote mbili, ambapo kwa upande wa Tanzania miongoni mwa
waliohudhuria na kushuhudia utiaji saini huo ni pamoja na Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi
(TVET), Dkt. Noel Mbonde; Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi, Peter Maduki; Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi (VETA), Dkt. Pancras Bujulu na Mkurugenzi Msaidizi wa TVET, Enock Kayani.
Akizungumza
wakati wa kutia saini makubaliano hayo, Dkt. Akwilapo alisema ujenzi huo unatarajiwa
kuanza mara moja na utachukua takribani
miezi 18 kukamilika na kwamba unaongeza mchango katika kuandaa nguvukazi kwa
ajili ya Uchumi wa Viwanda nchini.
Alisema,
baada ya kukamilika chuo hicho kitakuwa ana uwezo wa kudahili wanafunzi 400
katika kozi za muda mrefu na zaidi ya 1000 kozi za muda mfupi huku kikiwa na
nafasi za bweni 200 kwa wanafunzi wa kiume na 120 kwa wanafunzi wa kike.
Kwa
upande wake, Yuan Lin alisema kuwa ujenzi wa Chuo hicho ni sehemu ya
uendelezaji mahusiano mema kati ya China na Tanzania na kwamba unaonesha
uhalisia wa China kuunga mkono kwa vitendo juhudi za Tanzania kuelekea katika
uchumi wa viwanda.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt Pancras Bujulu licha ya kuishukuru serikali ya
China kwa msaada huo, alisema kuwa VETA kwa kushirikiana na serikali mkoani
Kagera tayari wameshaweka miundombinu muhimu kwa ajili ya kuwezesha shughuli za
ujenzi wa chuo hicho kuanza mara moja.
Aliitaja
miundombinu iliyoandaliwa kuwa ni pamoja na kuboresha barabara iendayo kwenye
eneo la ujenzi wa chuo kwa kuichonga na kuitengeneza kwa kiwango cha
changarawe; kuvuta umeme hadi kwenye eneo la ujenzi na kutengeneza chanzo cha
muda cha maji kwa ajili ya shughuli za ujenzi.
Aliongeza
kuwa wakati chuo hicho kikitarajiwa kuanza kujengwa, tayari walimu 20 kutoka
VETA wamekwenda nchini China kujifunza namna ya uendeshaji wa vyuo vya ufundi
stadi ikiwa ni sehemu mojawapo ya kuimarisha mahusiano katika uendeshaji wa
elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Alisema,
VETA inaendelea kuongeza juhudi za ujenzi na upanuzi wa vyuo na nia ni
kuhakikisha kila mkoa una chuo cha elimu na mafunzo ya ufundi stadi chenye
hadhi ya Kimkoa.
No comments:
Post a Comment