Mkurugenzi Mtendaji
wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku ameitaka Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kutumia vifaa vilivyopo katika karakana zake
kuchonga vipuli na kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa mahitaji mbalimbali nchini.
Butiku alitoa ushauri huo wakati wa mahafali
ya chuo cha VETA Dar es Salaam yaliyofanyika Novemba 23, 2018.
Alisema baada ya
kutembea kwenye karakana mbalimbali na kuhojiana na walimu na wanafunzi,
amebaini kuwa VETA ina rasilimali na hazina kubwa ya mashine na ujuzi wa walimu
na wanafunzi ambao ukitumiwa vyema unaweza kuzalisha vitu vingi ambavyo kwa
kiasi kikubwa bado vinafanywa na watu binafsi au kununuliwa kutoka nje ya nchi.
“nimejionea vifaa
vingi ambavyo naamini vikitumika vizuri vinaweza kuleta manufaa makubwa sana
kwa taifa, ifike mahali sasa vifaa mlivyonavyo katika karakana zenu viweze
kutengeneza mashine nyingine kwa ajili ya matumizi mbalimbali ” Alisema
Alitoa mfano wa karakana
ya uchapaji ambayo alisema ikiimarishwa inaweza kufanya shughuli nyingi sana za
uchapaji wa vitu mbalimbali kwa kuwa ina vifaa na wataalam muhimu vya kuweza
kufanya shughuli hizo kwa ufanisi mkubwa.
Sambamba na hilo,
aliishauri VETA kuanzisha masomo ya sanaa kama vile nyimbo na ngoma za asili kwa
kuwa sanaa hizo kwa sasa ni ajira kwa vijana na zikiwekewa utaratibu mzuri
zitakuwa na manufaa makubwa kwa nchi huku akiwaasa wahitimu kutumia vyema ujuzi
walioupata kujitengeneza ajira zao wenyewe kupitia vikundi.
Mkurugenzi Mkuu wa
VETA Dkt Pancras Bujulu alisema mamlaka hiyo inaendelea na juhudi mbalimbali za
kuhakikisha inazalisha mafundi stadi mahiri watakaoweza kukidhi mahitaji ya
soko la ajira na kushiriki kikamilifu katika miradi mbalimbali inayotekelezwa
na serikali ikiwa ni pamoja na mwelekeo kwenye uchumi wa viwanda.
Alivitaka vyuo vya
ufundi stadi kuweka nguvu katika kuendeleza vipaji vya vijana kwa kuwa vijana
wengi wanaosoma katika vyuo hivyo wana vipaji ambavyo vikiendelezwa vinaweza
kuwanufaisha na kuendelea.
Dkt. Bujulu alitumia
fursa hiyo pia kuwatangazia na kuwataka wahitimu, wanafunzi na walimu wenye
ubunifu kushiriki kwenye mashindano ya kitaifa ya sayansi, teknolojia na
ubunifu yaliyozinduliwa Novemba 14, yakiwa na lengo la kuibua vipaji na kuhamasisha uendelezaji wa
teknolojia na ubunifu utakaoweza
kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo endelevu ya viwanda, kuongeza tija
ya uzalishaji wa malighafi, kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini
pamoja na kuboresha shughuli nyingine za kiuchumi.
Aliwasihi wafanyakazi
wa VETA kutumia utaalam walionao kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika
vyuo kwa kutumia rasilimali zilizopo na kuongeza kuwa VETA itaendelea na
jitihada za kuhakikisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi inawafikia wananchi
wengi zaidi ili watanzania wengi wanufaike nayo .
Awali, Kaimu Mkuu wa
Chuo cha VETA Dar es Salaam Violeth Fumbo alisema jumla ya vijana 536
wamehitimu ambapo 523 wamehitimu ngazi
za ufundi stadi daraja la pili katika fani 20 za ufundi na 13 wamehitimu
Diploma ya Ubunifu wa nguo na mitindo ya mavazi.
Alisema pamoja na
wahitimu hao wa kozi za muda mrefu, chuo hicho kimeendelea kuboresha huduma
zake ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya muda mfupi kulingana na mahitaji na
kwamba kwa mwaka huu chuo hicho kimeweza kutoa wahitimu wa kozi za muda mfupi
10,300.
Naye mwakilishi wa
waajiri kutoka kampuni ya PLASCO Fidelis Mashauri alisema waajiri wamejenga
imani kubwa kwa vijana wanaotoka katika vyuo vya VETA kwa kuwa wanaonekana wamepikwa vyema na kuwa mahiri katika fani
zao.
No comments:
Post a Comment