Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeingia makubaliano na Shirika la Kimataifa la Care
na Asasi ya Ukuzaji Kilimo Uwanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) kutekeleza
mradi unaolenga kujenga na kuimarisha ujuzi katika sekta ya kilimo, hususani
kwa makundi maalum katika mikoa ya Iringa, Njombe na Morogoro.
Makubaliano ya
mradi huo uliopewa jina la Tajirika yalisainiwa jana, 28 Novemba 2018 katika
ofisi za VETA Makao Makuu na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt Pancras Bujulu, Afisa
Mtendaji Mkuu wa SAGCOT, Goeffrey Kirenga na Naibu Mkurugenzi wa Sera na
Programu wa Care nchini Tanzania , Gloria Cheche.
Mradi huo
unatarajiwa kuwanufaisha 2200 kutoka makundi maalum, ambapo kati yao 70% ni wa
kike kwa kuwapatia msaada wa kifedha na vifaa vya mafunzo ili waweze kuhudhuria
na kujifunza ufundi stadi.
Akizungumza
wakati wa kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras
Bujulu alisema ushirikiano huo unalenga kuimarisha ubora wa mafunzo ya ufundi
stadi na kuendeleza ujasiriamali katika eneo la kilimo kwa jamii za watu
waishio vijijini nchini Tanzania.
“Tumebaini
hitaji kubwa la ujuzi wa ufundi stadi kwenye sekta ya kilimo, maana kuna vijana
wengi wamekuwa wakijishughulisha na kilimo bila ya kuwa na ujuzi maarifa
sahihi. Kwa hivyo kunakuwa hakuna ufanisi na tija inakuwa ndogo,” alisema.
Alisema
Mamlaka sasa inaweka mipango na mikakati mbalimbali kuimarisha mafunzo katika
eneo la kilimo na ushirikiano na wadau hao wawili unachangia kwenye juhudi za
Mamlaka kutoa mafunzo yanayogusa kilimo.
Katika
kutekeleza mradi huo, VETA itaandaa mitaala, kufundisha walimu wa walimu, kutoa
mafunzo yenye lengo la kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia taarifa
za mahitaji ya soko katika kilimo.
Naibu
Mkurugenzi wa Sera na Programu wa Care nchini Tanzania , Gloria Cheche alisema
shirika lake lilivutiwa kushirikiana na VETA kwa kutambua kuwa kupitia VETA ni
rahisi kuwapata vijana wengi nchini.
“tunatambua
pia kuwa kwa kufanya kazi na VETA ni rahisi pia kuwafikia watu wa makundi maalum katika jamii na kuwawezesha
kujikwamua kimaisha kwa kuwafundisha ujuzi
wa kuajirika,” alisema.
Alisema Care
International ambayo itakuwa ndio msimamizi na mratibu mkuu wa mradi, pamoja na
mambo mengine, itawashirikisha wadau wote na kujenga mahusiano mazuri na
serikali kuu na serikali za mtaa katika kutekeleza mradi katika maeneo husika.
Afisa Mtendaji
Mkuu wa SAGCOT Goeffrey Kirenga alishukuru kuanza kwa ushirikiano huo akisema
kuwa kilimo kinaendelea kupanuka sambamba na mahitaji ya ujuzi katika
sekta hilo.
Alisema
ushirikiano ulioanzishwa utasaidi kushughulikia changamoto za mahitaji ya ujuzi,
hasa kwenye maeneo ya usindikaji na uhifadhi wa mazao ya kilimo.
Katika mradi
huo ambao mafunzo yatatolewa zaidi kwenye jamii, SAGCOT itachangia katika kutoa
taarifa za mahitaji ya soko la ajira kwenye eneo la kilimo, hasa mtazamo wa
sekta binafsi pamoja na vipaumbele vinavyoweza kuingizwa kwenye mitaala ili
wahitimu waweze kuajirika kwa urahisi.
No comments:
Post a Comment