Mratibu wa Idara ya
Maendeleo Vijana na Chipukizi wa Chama cha Wasiiona Tanzania, Kiongo Itambu ameiomba
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuhuisha mitaala yake ili iweze
kuwa rafiki zaidi kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa watu wenye uelemavu wa aina
zote hasa wasioona.
Itambu alisema hayo jana
Novemba 29, 2018 wakati akipokea hundi ya Shilingi laki tano kutoka VETA kwa
ajili ya kuwezesha kiongozi mmoja wa chama hicho kuhudhuria maadhimisho ya siku
ya watu wenye ulemavu itakayofanyika Desemba 1, 2018 mkoani Simiyu.
Alisema chama hicho
kinatambua mchango wa VETA katika kuwapatia vijana ujuzi na kwamba watu wengi
zaidi wenye ulemavu wakipata ujuzi huo utawasaidia kuinua uchumi wao na
kuchangia pato la taifa.
“Tunaomba sana VETA
iwaangalie kwa jicho la pili watu wenye ulemavu ili nao waweze kupata fursa
zaidi ya kupata elimu ya ufundi stadi kwa kuandaa mitaala na mazingira rafiki
ya kufundishia” Alisema
Aliishukuru VETA kwa
msaada huo na kuomba Mamlaka hiyo iendelee kushirikiana nao kwa karibu katika
shughuli mbalimbali wanazozifanya.
Naye Afisa Uhusiano
wa VETA Dora Tesha alimsihi kiongozi huyo kutumia majukwaa mbalimbali na
mikutano ya vyama vya wenye ulemavu kuwafahamisha watu hao juu ya fursa zilizopo
katika vyuo vya Ufundi stadi nchini na kuwahamasisha kuzitumia vyema kupata
ujuzi na kuweza kujiajiri wenyewe.
Alisema VETA imekuwa
ikitoa mafunzo kwa watu wenye ulemavu ingawa idadi kubwa ya wanaojitokeza ni
wenye ulemavu wa viungo ambapo kwa mwaka 2017 jumla ya vijana wenye ulemavu 334 walipata mafunzo katika fani mbalimbali katika vyuo vya ufundi stadi na
kwamba kati yao 214 ni wenye ulemavu wa viungo na 11 pekee ndiyo wasiiona.
Alimuomba kiongozi
huyo kuialika VETA kwenye makongamano na mikutano mbalimbali inayowakutanisha
watu wenye ulemavu ili kuweza kutoa elimu juu ya fursa zilizopo katika vyuo vya
Ufundi stadi na kufafanua hoja mbalimbali.
No comments:
Post a Comment