Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesaini makubaliano ya kuanzisha
ushirikiano kati yake na Chuo cha Henan cha Ufundi Stadi wa Kilimo lengo la
kuboresha utoaji wa mafunzo kwa njia ya kutembeleana na kubadilishana ujuzi na
maarifa kwa walimu na wanafunzi na shughuli zingine za kitaaluma.
Makubaliano
hayo ya awali yaliafikiwa na kusainiwa (tarehe 20 Desemba 2018) kati ya Makamu
wa Rais wa Chuo cha Henan cha Ufundi Stadi wa Kilimo, Profesa Dou Ruimu kwa
upande mmoja na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dr. Pancras Bujulu kwa upande mwingine
na kwamba yatafuatiwa na utiaji saini wa Waraka wa Makubaliano (MoU) siku za
mbeleni.
Utiaji saini
wa makubaliano ya awali uishuhudiwa na Mkurugenzi wa Mafunzo na Ufundi Stadi
(TVET), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Noel Mbonde na Mwenyekiti
wa Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET Board), Peter Maduki,
wawakilishi wa Chuo cha Henan na Wajumbe wa Menejimenti ya VETA.
VETA ina nia
ya kuimarisha mafunzo katika sekta ya kilimo na miongoni mwa malengo yake ni
kukiimarisha na kukiboresha chuo cha VETA Kihonda ili kiweze kubobea na kuwa
kituo bora cha mfano katika mafunzo ya ufundi stadi kwenye sekta ya kilimo.
Kabla ya
kusaini makubaliano, ujumbe wa watu sita kutoka Chuo cha Henan cha Ufundi Stadi
wa Kilimo ukiwahusisha watendaji wakuu na wataalam mbalimbali umekuwepo nchini
tangu Jumanne tarehe 18 Desemba 2018 ambapo ulifanya majadiliano na Menejimenti
ya VETA Makao Makuu, ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt Pancras Bujulu na Jumatano,
tarehe 19 Desemba 2018 ulitembelea ofisi ya VETA Kanda ya Mashariki, kisha chuo
cha VETA Kihonda na kujionea karakana, mashine na vifaa mbalimbali
vinavyotumika kufundishia fani ya Ufundi wa Zana za Kilimo (Agro-mechanics),
mafunzo ambayo yanagusa sekta ya kilimo ambayo ndio mkondo wa chuo cha Henan.
Akizungumza
kabla ya kutiwa saini makubaliano hayo ya awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET Board), Peter Maduki alisema Bodi yake
inaunga mkono ushirikiano huo kutokana na kutambua umuhimu wake wa uwezekano wa
kuchangia kuboresha mafunzo kwenye sekta ya kilimo ambayo ni ya msingi katika
uchumi wa nchi.
“Zaidi ya
asilimia 70 ya wa Watanzania wanategemea kilimo, kwa hivyo kuboresha mafunzo
kwenye kilimo maana yake ni kuboresha maisha ya Watanzania,” alisema.
Aliongeza kuwa
hata katika mkakati wa sasa wa nchi kuelekea kwenye uchumi wa viwanda,
kuboreshsa ujuzi katika kilimo ni sawa na kuhakikisha upatikanaji wa malighafi
kwa ajili ya viwanda kwa kuwa viwanda vingi vya nchi zinazoendelea kama
Tanzania hutegemea zaidi malighafi kutokana na mazao ya kilimo.
Vilevile,
Mkurugenzi wa Mafunzo na Ufundi Stadi (TVET), Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Dkt. Noel Mbonde aliahidi kusaidia uharakishwaji wa ushirikiano huo
kwa kuwa una fursa kubwa ya kuboresha utoaji wa mafunzo ambao ndio eneo
analosimamia.
Kwa sasa
mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vinavyomilikiwa na visivyomilikiwa na VETA
hutolewa katika kozi za Ufundi wa Zana za Kilimo, Teknolojia ya Usindikaji wa
Nyama, Usindikaji wa Mbegu za Mafuta, Kilimo cha Bustani na Mazao ya Nafaka,
Uhudumu wa Misitu, Uokaji, Kilimo cha Uyoga, Utengenezaji wa Mvinyo, Usindikaji
wa Mboga na Matunda, Usindikaji wa Samaki na Usindikaji wa Asali.
Kwa upande
mahsusi wa vyuo vinavyomilikiwa na VETA, mafunzo ya muda mrefu ambayo ni ya
kipindi cha miaka miwili hadi mitatu hutolewa katika fani za Ufundi wa Zana za
Kilimo
(VETA Kihonda, VETA Manyara, VETA Arusha-Oljoro, VETA Mpanda na VETA Dakawa); Ufugaji
(VETA Singida); Teknolojia ya Usindikaji wa Nyama (VETA Dodoma). Vilevile VETA
huendesha kozi za muda mfupi ambazo ni za kati ya miezi miwili hadi sita
kupitia programu yake ya Uboreshaji Ujuzi kwa Wajasiriamali kwenye Sekta Isiyo
Rasmi (INTEP) ukihusisha mafunzo mbaimbali kama Kilimo cha Uyoga, Ufugaji wa
Samaki, Utengenezaji Mvinyo, Usindikaji
wa Mboga na Matunda, Usindikaji wa Samaki na Usindikaji wa Asali.
Chuo cha Henan
cha Ufundi Stadi wa Kilimo (Henan Vocational College of Agriculture)
kilianzishwa mwaka 1952. Chuo hicho kilichopo katika jimbo la Henan
kinachomilikiwa na serikali ya China ni chuo cha mfano katika utoaji wa elimu
ya ufundi stadi katika fani ya kilimo ikiwa ni pamoja na kilimo cha bustani na
mbogamboga, ufugaji na usindikaji wa chakula.
No comments:
Post a Comment