Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) iko katika majadiliano na Chuo cha
Henan cha Ufundi Stadi wa Kilimo cha nchini China (Henan Vocational College of
Agriculture) kuona uwezekano wa kushirikiana katika utoaji mafunzo ya ufundi
stadi katika sekta ya kilimo nchini.
Ujumbe wa watu
sita kutoka Chuo cha Henan cha Ufundi Stadi wa Kilimo ukiwahusisha watendaji
wakuu na wataalam mbalimbali umekuwepo nchini tangu jana, Jumanne tarehe 18
Desemba 2018 ambapo ulifanya majadiliano na Menejimenti ya VETA Makao Makuu,
ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt Pancras Bujulu.
Leo Jumatano, tarehe 19 Desemba 2018 ujumbe
huo ulitembelea ofisi ya VETA Kanda ya Mashariki, kisha chuo cha VETA Kihonda
na kujionea karakana, mashine na vifaa mbalimbali vinavyotumika kufundishia
fani ya Ufundi wa Zana za Kilimo (Agro-mechanics), mafunzo ambayo yanagusa
sekta ya kilimo ambayo ndio mkondo wa chuo cha Henan.
Miongoni mwa
maeneo muhimu ya ushirikiano ambayo VETA inayapendekeza ni kuimarisha chuo cha
VETA Kihonda ili kiweze kubobea na kuwa kituo bora cha mfano katika mafunzo ya
ufundi stadi kwenye sekta ya kilimo.
Mambo mengine
ni kubadilishana teknolojia, mafunzo kwa walimu, na kutembeleana kwa walimu na
wanafunzi kwa ajili ya kubadilishana ujuzi na maarifa (exchange visits).
Kesho,
Alhamisi ujumbe huo unatarajiwa kukutana na kufanya majadiliano na viongozi
waandamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Peter Maduki.
Chuo cha Henan
cha Ufundi Stadi wa Kilimo (Henan Vocational College of Agriculture)
kilianzishwa mwaka 1952. Chuo hicho kilichopo katika jimbo la Henan
kinachomilikiwa na serikali ya China ni chuo cha mfano katika utoaji wa elimu
ya ufundi stadi katika fani ya kilimo ikiwa ni pamoja na kilimo cha bustani na
mbogamboga, ufugaji na usindikaji wa chakula.
No comments:
Post a Comment