Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameahidi kushughulikia
changamoto ya uchakavu wa miundombinu katika vyuo vya ufundi stadi
vinavyomilikiwa na VETA ili kuwezesha utoaji wa mafunzo bora sambamba na
mabadiliko mbalimbali ya teknolojia viwandani na kukidhi viwango vya mahitaji
ya waajiri.
Prof.
Ndalichako alitoa ahadi hiyo kufuatia ombi la Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Pancras Bujulu wakati akitoa
maelezo mafupi kabla ya kumkaribisha kutoa hotuba kwenye sherehe za mahafali ya
33 ya Chuo cha VETA Moshi yaliyofanyika chuoni hapo Jumatano, 12 Desemba 2018.
Katika
maelezo yake, Dkt. Bujulu alisema kuwa baadhi ya vyuo vya VETA ni vikongwe mno
na miundombinu yake imechakaa sana, hivyo ukarabati wake kwa kutumia fedha
ambazo VETA imekuwa ikipatiwa na serikali umekuwa ni mgumu.
Alisema
pamoja na uchakavu wa miunndombinu kwa ujumla vifaa na mashine zinazotumika
kwenye karakana kwa ajili ya kufundishia pia zimechakaa na zingine zimepitwa na
wakati kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia hivyo hazifai kutumika
kufundishia ili kutoa mafundi wanaokidhi mahitaji ya wakati huu.
“Nikizingatia
uzoefu wangu na wewe kuwa una mapenzi sana na miundombinu ya vyuo. Umetengeneza
catalogue ya kutengeneza miundombinu ya vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu.
Naomba sasa na hivi vya stadi za kawaida navyo utengeneze catalogue (mchanganuo
wa mahitaji) ili uwe unajua chuo chetu cha wapi na wapi na wapi kinahitaji nini
na utakuwa unajua wapi unapata hela kidogo unatengeneza,” alisema.
Akijibu
ombi hilo, Prof. Ndalichako alisema kuwa alisema kwa kutambua jukumu na shauku
ya kutaka taasisi zilizo chini yake zinakwenda vizuri, alisema kuwa yuko tayari
kupokea mchanganuo wa mahitaji ya vyuo vya ufundi stadi nchini ili ayafanyie
kazi.
“Mkiniwezesha
nikafahamu vizuri mahitaji yenu, na kwa sababu ni kipaumbele cha serikali ya
awamu ya Tano, na Mheshimiwa Rais (John Pombe Magufuli) amekuwa akisisitiza
hili eneo la mafunzo ya ufundi stadi niweze kuliimarisha vizuri, basi nina kila
sababu ya kuhakikisha ninasikiliza ushauri wa wataalam ili tuweze kuhakikisha
kuwa tunaimairisha mafunzo ya ufundi stadi kwa kiwango ambacho ndio
kinahitajika na wataalam wetu na kinachokubalika na waajiri ambao huwachukua
vijana wanapomaliza mafunzo,” alisema.
Alisema
kuwa elimu ya ufundi stadi ina umuhimu sana katika kipindi hiki ambacho
serikali imeweka mikakati ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi
unaoendeshwa, kwani hakuna kiwanda kinachoweza kuendeshwa bila mafundi stadi.
Wakati
huohuo, Prof. Ndalichako ameiagiza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi
(VETA) kwa kushirikiana na Idara ya Ufundi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia pamoja na Chemba ya Madini na Nishati (TCME) na wadau wengine kukaa
na kuweka utaratibu wa kupanua Mpango wa Mafunzo ya Uanagenzi katika vyuo
vingine vya VETA nchini na kushirikisha sekta zingine zaidi ya madini.
Alisema,
mfumo wa mafunzo kwa njia ya uanagenzi una manufaa makubwa kwa pande zote,
akifafanua kuwa licha ya kusaidia kuongeza udahili, mfumo huu unasaidia vijana
kujifunza teknolojia mpya zilizopo viwandani; kusaidia vijana kupata ujuzi na
uzoefu halisi unaohitajika mahala pa kazi katika fani husika na makampuni kuwa
na uhakika wa nguvukazi yenye umahiri wa kiwango wanachokihitaji.
Mahafali
ya 33 ya chuo cha VETA Moshi yalihusisha jumla ya wahitimu 174 wa fani
mbalimbali wakiwemo daraja la 2 (yaani level 2) 104, Daraja la 3 (yaani Level
3) 24 na wanagenzi kupitia mradi wa IMTT ni 46.
No comments:
Post a Comment