Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amehitimisha ziara yake ya
ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi Kanda
ya Ziwa huku akiwataka wakandarasi kutekeleza wajibu wao kwa juhudi na uadilifu
ili kuhakikisha wanakamilisha ujenzi kwa wakati kulingana na mikataba ya miradi
husika.
Katika ziara yake
Kanda ya Ziwa tangu tarehe 24 hadi 26 Januari 2019, Profesa Ndalichako
alitembelea miradi mitatu ya ujenzi wa vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi
stadi vikiwemo Chuo cha VETA cha Mkoa wa Geita, Chuo cha VETA cha Wilaya ya Chato,
Chuo cha VETA cha Bukoba kwa ajili ya Mkoa wa Kagera pamoja na mradi wa
ukarabati wa Chuo cha Ufundi Stadi Karagwe kinachomilikiwa na Halmashauri ya
wilaya ya Karagwe.
Prof. Ndalichako
alifurahishwa na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa Chuo cha VETA cha wilaya ya
Chato unaofanywa na kampuni ya CF Builders na kusema kuwa ni vyema wakandarasi
wanaoonesha juhudi na uadilifu katika kazi zao wakaendelea kupewa kazi katika
miradi mingine inayojitokeza badala ya kuchukua wengine ambao utendaji kazi wao
hauna uhakika.
“Nimpongeze sana huyu
mkandarasi CF Builders ambaye pia ndiye aliyejenga chuo cha ufundi stadi
Namtumbo ambako kwa kweli nako pia alifanya kazi nzuri na akamaliza kwa wakati.
Niseme kwamba, watu wa manunuzi wawe na uzalendo. Mtu anayefanya kazi nzuri kama
huyu kama anafanya kazi nzuri kwa nini hata kama kuna site (eneo au mradi)
nyingine wasimpe?” alisema na kuhoji.
Alisema kuwa wakati
kwa mujibu wa mkataba mradi huo unatakiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu,
hadi siku ya tarehe 24 Januari mwaka huu mkandarasi alikuwa mbele kwa asilimia
3.6 na kwamba matarajio yake ni kukamilisha na kukabidhi mradi ifikapo Julai
mwaka huu.
Mwakilishi wa
Mkandarasi wa CF Builders, Fred Chacha alisema kuwa kampuni yao pia ilijenga na
kukamilisha vyema vyuo vya VETA Singida, VETA Mara na VETA Namtumbo na ilipata
ushirikiano mzuri wa VETA na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Kwa kuthamini
ushirikiano huo na kutokana na ombi la Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt, Pancras
Bujulu, CF Builders imeahidi kutoa msaada wa ujenzi wa jengo moja kwa ajili ya
kituo cha huduma ya kwanza ndani ya chuo cha VETA Chato.
Aidha, Prof.
Ndalichako alionesha imani na mwenendo wa mradi wa ukarabati wa Chuo cha Ufundi
Stadi Karagwe unaofanywa na Wakala wa Ujenzi Tanzania (TBA) na kuwa na matumaini
kuwa nao utakamilika kwa wakati.
Hata hivyo, Waziri
Prof. Ndalichako alishuhudia kusuasusa kwa maendeleo ya mradi wa ujenzi wa chuo
cha VETA cha Mkoa wa Geita unaofanywa na kampuni ya Skywards Construction na
kumtaka mkandarasi kuongeza kasi ya utendaji ili kufanikiwa kukamilisha ujenzi
mwezi Agosti mwaka huu kulingana na makubaliano yaliyopo kwenye mkataba.
Alisema kuwa
upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi unapaswa kupewa kipaumbele cha
hali ya juu kwani ni nguzo muhimu katika kusaidia maendeleo ya viwanda ambao
ndio mwelekeo wa serikali ya awamu ya tano na ndio maana yeyote anayekwamisha
juhudi za kupanua fursa za mafunzo hayo kupitia ujenzi na upanuzi wa vyuo
hapaswi kuvumiliwa.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt
Pancras Bujulu alisisitiza kauli ya Waziri juu ya umakini katika taratibu za
zabuni na manunuzi ili kupata wakandarasi sahihi wenye kufanya kazi kwa umakini
na uadilifu.
Aliwaomba wakandarasi
wengine pia kujituma na kuthamini na kuzingatia umuhimu wa kusimamia vyema
miradi yao ili iweze kukamilika kwa ufanisi.
Katika mikoa ya Kanda
ya Ziwa, VETA inasimamia Ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Geita wenye
thamani ya Sh. 9.9 na fedha zinazogharamia mradi huo zinatokana na mkopo kutoka
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB); ujenzi wa Chuo cha VETA cha Wilaya ya
Chato wenye thamani ya Sh. bilioni 10.7 ambazo ni fedha za ndani; ujenzi wa
chuo cha VETA cha Mkoa wa Kagera wenye thamani ya Sh. bilioni 20 ambao
unagharamiwa na Serikali ya China na ukarabati wa Chuo cha Ufundi Stadi Karagwe
wenye thamani ya Sh. bilioni 4.6 fedha za ndani.
No comments:
Post a Comment