Tarehe
ya leo 14 Februari ambayo huadhimishwa kama Siku ya Wapendanao (maarufu kama
Valentine) imekuwa njema kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
kwani imeambatana na tukio muhimu la Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, mkoani
Pwani kutoa jumla ya ekari 200 kwa VETA ambalo litasaidia kupanua shughuli za
utoaji elimu na mafunzo ya ufundi stadi, hususani kwa vyuo vya VETA vilivyoko
Dar es Salaam.
Akizungumza
kabla ya makabidhiano ya eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mheshimiwa
Jokate Mwegelo alisema ni bahati kubwa kwa VETA kupata eneo hilo ambalo limekaa
kimkakati kutokana na kuwa na miundombinu muhimu na kuzungukwa na maeneo muhimu
kiuchumi.
Alisema,
eneo hilo lililopo kwenye kitongoji cha Kazimzumbwi, kata ya Kazimzumbwi halmashauri
ya Kisarawe mji liko kandokando ya barabara inayotoka Kisarawe mjini kwenda
kwenye Pori la Hifadhi la Selous ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami na
kwamba Reli ya Kati, Standard Gauge na TAZARA pamoja na mradi wa maji kwa ajili
ya wilaya ya Kisarawe vyote vinapita eneo hilo.
Vilevile,
alisema eneo hilo liko jirani na ukanda maalum wa kiuchumi (special economic
zone), ambao unaweza kutoa fursa kwa vijana kupata maeneo ya kufanyia mazoezi
ya vitendo na ajira baada ya kuhitimu mafunzo yao.
“Mkoa
wa Pwani tumejipambanua kama mkoa wa viwanda. Lakini ili viwanda viwanufaishe
vyema wananchi wa Kisarawe kuna mahitaji makubwa kwa vijana kupata ujuzi kwa
ajili ya kufanya kazi kwenye viwanda. Kwa hiyo tunaona ni jambo la msingi VETA
waje watusaidie kuinua ujuzi kwa vijana na watu wetu. Tunahitaji nguvukazi
yenye ujuzi,”alisema.
Alisema,
ni matumaini yake kuwa baada ya VETA kukabidhiwa eneo hilo watafanya juhudi za
haraka kuanza kuliendeleza.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu aliushukuru uongozi wa Wilaya na
Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kwa kuwa tayari na kwa wepesi kutoa eneo hilo
kwani litasaidia kwa kiasi kikubwa kupanua shughuli za mafunzo ya VETA,
hususani kwa kanda ya Dar es Salaam.
Alisema,
vyuo vya VETA vya Dar es Salaam (Chang’ombe) na Kipawa viko katika maeneo
madogo sana ambapo vimejibana na kukosa nafasi za kupanua huduma zao, kwa hiyo
kupatikana kwa eneo hilo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupanua mafunzo ya vyuo
hivyo.
Alisema,
wapo pia wadau ambao wameonesha nia ya kushirikiana na VETA kutoa mafunzo
katika maeneo mbalimbali kama kilimo, usafirishaji na TEHAMA lakini jambo la
nafasi lilikuwa linaonesha dalili ya kuwa kikwazo.
Aliongeza
kuwa eneo hilo linaweza kusaidia hata kujenga mabweni ya wanafunzi wa vyuo vya
VETA Dar es Salaam na Kipawa ambavyo vyote viwili havina mabweni, hivyo
wanafunzi wote wa vyuo hivyo wanahudhuria mafunzo kwa kutwa.
No comments:
Post a Comment