Naibu Waziri wa Elimu
Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa William Tate Olenasha, leo tarehe 5 Machi
2019, amefungua rasmi mashindano ya sayansi, teknolojia na ubunifu ngazi ya
kitaifa katika viwanja vya Kumbukumbu ya Nyerere (Nyerere Square) jijini
Dodoma, huku akiwataka wadau mbalimbali kushirikiana na serikali katika
kuhamasisha harakati za sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuongeza mchango
katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mashindano ya mwaka
huu yanaongozwa na kaulimbiu, “Kukuza Ujuzi na Ubunifu kwa Uchumi wa Viwanda,”
na yamehusisha makundi mbalimbali ya wabunifu na wadau wa sayansi, teknolojia
na ubunifu katika maeneo na nyanja mbalimbali nchini kote.
Mheshimiwa Ole Nasha
amepongeza utaratibu wa kuanzisha mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia
na Ubunifu, akisema kuwa utaratibu wa kuwabaini na kuwashindanisha wabunifu ni
miongoni mwa mambo yanayoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuhamasisha na
kuleta mwamko zaidi ili kuibua na kuendeleza teknolojia na ubunifu miongoni mwa
Wananchi.
“Hivyo, ni vyema
tukaweka mipango na mikakati ya kudumisha utaratibu huu wa kuwa na Mashindano
ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kila mwaka. Licha ya kuleta mwamko
zaidi kwa wabunifu, jambo hilo linaweza kuwa chachu ya kuhamasisha matumizi ya teknolojia
bora miongoni mwa wananchi,” alisema.
Wakati akitembelea
maonesho ya wabunifu, Naibu Waziri alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Daktari
Pancras Bujulu kufanya mazungumzo na taasisi na mamlaka husika ikiwemo Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kuhusiana na
ubunifu wa Mfumo wa Kudhibiti Ajali kwenye Makutano ya Reli na Barabara
uliofanywa na Mwalimu Emmanuel Bukuku wa VETA Dar es Salaam na Ubunifu wa
Kudhibiti wa Ajali za Pikipiki uliofanywa na Mwalimu Aneth Mganga wa VETA
Kipawa ili kuhakikisha kuwa ubunifu unafika katika matumizi halisi kwenye
jamii.
Aidha, Mheshimiwa
Naibu Waziri Ole Nasha aliagiza kuboresha mchakato wa utaratibu wa kupata
wabunifu kutohusisha maandiko ya kitaalam sana, badala yake iwe ni kuwafuata
wabunifu na kuwafanyia tathmini huko waliko.
Akitoa maelezo mafupi
kuhusu mashindano, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Prof. James Mdoe, alisema mashindano hayo yamepitia katika mchujo uliohusisha
makundi na ngazi mbalimbali kote nchini ukiratibiwa na Wizara kupitia Tume ya
Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH); Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam
(DIT); na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
“Mchakato wa
mashindano hayo ulianza kwa kupokea maombi ya wabunifu na kusajili kuanzia
tarehe 10 Januari 2019 hadi 17 Februari 2019. Jumla ya wabunifu 415
walijisajili kutoka: Vyuo Vikuu na taasisi za utafiti (53); Vyuo vya Ufundi
Sanifu (27); Vyuo vya Ufundi stadi na Sekta Isiyo Rasmi (262); na Shule za
Sekondari (78),” Alisema.
Alisema, mashindano
katika ngazi ya kitaifa yatafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 5 hadi 7 Machi
2019 na yatahusisha jumla ya wabunifu 60 watakaoonesha ubunifu wao na kufanyiwa
tathmini ya mwisho ili kupata washindi watatu bora kutoka kila kundi watakaopewa
tuzo siku ya kilele
Alisema wabunifu
wanaoshiriki katika fainali za mashindano wamebuni na kutengeneza vitu na
mawazo yanayolenga kutatua changamoto mbalimbali katika sekta za afya, TEHAMA,
elimu, mifugo, kilimo, nishati, viwanda, mazingira, maji na umwagiliaji,
usafirishaji, madini, na maliasili.
Kilele cha Mashindano
hayo ni tarehe 7 Machi, 2019, ambapo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako anatarajiwa kufunga na kutoa tuzo kwa
washindi tatu bora wa kila kundi.
No comments:
Post a Comment