Katika hali
inayoashiria nia ya dhati ya kuendeleza
ujuzi, Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara imekabidhi majengo na
miundombinu mbalimbali ya chuo cha ufundi stadi Simanjiro kwa Mamlaka ya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ili kukiendesha na kukisimamia.
Makabidhiano hayo
yamefanyika tarehe 12 Machi 2019 katika kijiji cha Emboreet, kata ya Emboreet
na kutiwa saini na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro,
Yefred Myenzi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Jackson Sipitieck
kwa upande mmoja na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu kwa upande
mwingine.
Makabidhiano hayo
yamehusisha majengo yaliyokamilika yakiwemo madarasa matano; nyumba ya mwalimu
(Two in one); hosteli yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 48; miundombinu ya maji
safi ikihusisha kisima kirefu
kinachoendeshwa kwa umeme wa jua; matanki yenye ujazo wa lita 20,000; pamoja na
pampu inayosukuma maji kwa nguvu za umeme wa jua ikiwa na uwezo wa kujaza lita
6000 kwa saa.
Ujenzi wa karakana na
ununuzi wa vifaa vya kufundishia kozi ya awali ambayo ni Uashi unaendelea kwa
msaada wa Asasi ya ECLAT Foundation ya Simanjiro na Upendo ya Ujerumani.
Wakati ikikabidhi
majengo na miundombinu hiyo, Halmashauri ya Simanjiro inaendelea na taratibu za
kuomba hati miliki ya eneo la ukubwa wa ekari 104 ambalo miundombinu hiyo imo
ili hatimaye nayo iikabidhi kwa VETA, hivyo kuwezesha upanuzi shughuli mbalimbali
za utoaji mafunzo.
Mkurugenzi Mkuu wa
VETA Dkt. Pancras Bujulu aliwashukuru wananchi wa kata ya Emboreet kwa mwamko
waliouonesha katika kutambua na kuthamini elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Katika kuonesha VETA
kuunga mkono juhudi za wananchi wa wilaya hiyo, Dkt. Bujulu aliahidi kujenga
bweni moja la wavulana lenye uwezo wa kulaza wanafunzi 48 ili bweni lililopo
(ambalo nalo linaweza kulaza wanafunzi 48) litumike kwa wanafunzi wa kike.
Hati ya makabidhiano
ya eneo hilo imefafanua kuwa Halmashauri ya Simanjiro imejielekeza katika
kuwajengea vijana wahitimu ujuzi na ufundi stadi ii waweze kujiajiri na kwenda
sambamba na kasi ya maendeleo ya serikali ya Tanzania.
“Malengo ya
makubaliano haya kati ya Halmashauri na VETA ni kuendeleza viwango vya mafunzo
ya ufundi stadi na utoaji elimu kuzingatia viwango vya kitaifa,” inafafanua
sehemu ya Hati hiyo.
No comments:
Post a Comment