Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli jana Aprili, 5 2019 amezindua Chuo cha Ufundi Stadi
cha Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma huku akiupongeza uongozi wa Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi(VETA) kwa jitihada zake katika kupanua fursa
za elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Akihutubia
wananchi baada ya uzinduzi katika eneo la chuo hicho, Rais Magufuli alisema
kuwa VETA imeweza kujenga vyuo vingi katika kipindi kifupi sambamba na kubuni
namna zingine za kupanua fursa za elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
“mmejenga
vyuo vingi, hilo ni lazima niseme kwa dhati, kila mahali sasa kuna vyuo vingi
vinajengwa na mmejitahidi katika kipindi kifupi,” alisema.
Alizitaja
jitihada zingine zilizofanywa kuwa ni pamoja kurasimisha ujuzi uliopatikana nje
ya mfumo rasmi wa mafunzo na mafunzo ya uanagenzi yanayohusisha vyuo na mahala
pa kazi hivyo kusaidia vijana kupata muda mwingi wa mafunzo kwa vitendo.
Aliwakumbusha
wananchi juu ya umuhimu wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi katika kipindi hiki
akieleza kuwa nchi ya Tanzania sasa inaelekea kwenda kwenye uchumi wa kati
unaoongozwa na viwanda na hivyo inahitaji nguvukazi yenye ufundi stadi ambayo huandaliwa
na vyuo vya ufundi stadi vikiwemo vyuo vya VETA.
Hata
hivyo, Rais Magufuli aliiagiza VETA kufikiria juu ya kupunguza gharama za
ujenzi na ukarabati wa vyuo kwa kutumia nguvukazi ya ndani.
“Inawezekana
siku nyingine mnaweza kujifunza kwa kujenga kwa force account (nguvu ya ndani). Mkaichukua kama emergency (dharura) na kama trial
(majaribio) ya VETA yenyewe, mkawapa hawa vijana wa VETA na ninyi mkawa
consultants (washauri elekezi). ………….Na mimi nitawalinda kama kukitokea audit
query (hoja ya ukaguzi),” alisema.
Kwa
upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknojolia, Mhe. Prof. Joyce
Ndalichako katika maelezo yake kabla ya kumkaribisha Rais alieleza kuwa taratibu
za ununuzi wa vifaa kwa ajili ya chuo cha VETA Namtumbo zinaendelea ikiwemo
utengenezaji wa samani ambao unafanywa na Chuo cha Ufundi Stadi cha VETA Mbeya.
Alisema chuo hicho kinatarajiwa kutoa
mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi katika fani za Ufundi wa Maabara; Compyuta;
Uashi; Umeme wa majumbani na Vifaa vya Umeme (Electronics), Ufundi Bomba;
Ushonaji; Useremala na ufundi wa Mitambo Mizito.
Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, Chuo
hicho kina uwezo wa kudahili wanafunzi 900 kwa mwaka ambapo wanafunzi 175 ni wa
mafunzo ya muda mrefu kwa ngazi ya kwanza na wanafunzi 175 kwa ngazi ya pili na
600 wa mafunzo ya muda mfupi.
Awali
baada ya kupewa fursa kuzungumza, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Huduma za Jamii, Mhe. Juma Nkamia aliupongeza uongozi wa VETA kwa kazi nzuri na
kuahidi kuwa kutokana na kuridhishwa na utendaji kazi wa VETA, Kamati yake
itakuwa tayari kuidhinisha fedha mara moja muda wowote ikitokea kuna maombi ya
fedha kwa ajili ya shughuli za VETA.
No comments:
Post a Comment