Timu ya
wataalam kutoka Afrika Kusini imevutiwa na namna Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi (VETA) inavyotekeleza mpango wa Urasimishaji Ujuzi uliopatikana
nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo (RPL) na kuahidi kujipanga kwa ajili ya kuanzisha
ushirikiano na VETA katika eneo hilo.
Wajumbe wa
timu ya Wakala wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana nchini Africa Kusini (NYDA)
walibainisha hayo baada ya kupata maelezo ya utekelezaji wa mpango huo nchini
wakati wa kikao chao na Menejimenti ya VETA walipotembelea Makao Makuu ya VETA
jijini Dar es Salaam, tarehe 2 Aprili 2019 wakati wa ziara yao iliyokuwa chini
ya uenyeji na uratibu wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).
Mkurugenzi Mtendaji
wa NYDA, Ankie Motsoahae alisema kuwa wamevutiwa sana na maelezo ya namna VETA
inavyoendesha mpango wa RPL na kusema kuwa ingawa nchini Afrika kusini kuna mpango
kama huo, lakini utekelezaji haujafanyika kwa kipindi kirefu, hivyo mpango
umebaki kwenye nyaraka pekee.
“Kwangu mimi
RPL ni jambo la kuondoka nalo. Kama sehemu ya ushirikiano wetu na Tanzania,
tungependa kupata uzoefu kuhusiana na RPL. Tunatarajia kuja tena ndani ya miezi
miwili ili kurasimisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali.” Alisema.
NYDA ina
majukumu ya kuendeleza vijana nchini Afrika Kusini na elimu ni miongoni mwa
sekta za kipaumbele katika kuwaendeleza vijana. Timu hiyo ya NYDA ilifika nchini kwa ajili ya
kubainisha maeneo ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu na
ilitembelea baadhi ya taasisi nchini zikiwemo VETA; Tume ya Taifa ya Sayansi na
Teknolojia (COSTECH); Baraza la Michezo Tanzania (BMT); Baraza la Sanaa
Tanzania (BASATA); Wakala wa Huduma za Ajira (TaESA); Taasisi ya Sanaa na
Utamaduni Bagamoyo (TASUBA); Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Chuo
Kikuu cha Mzumbe.
Niapongeza VETA kwa kujiimarisha katika kupanua mpango huu wa urasimishaji wa ujuzi uliopatikan nje ya mfumo rasmi wa mafunzo. ILO itaendelea kushirikiana na nyi katika kuboresha viwango na utaalam katika eneo hili.
ReplyDelete