Waajiri
wa sekta ya umma nchini wamekumbushwa umuhimu wa kushirikisha wafanyakazi
katika kujadili, kupanga na kufanya maamuzi ya mambo mbalimbali katika taasisi
zao.
Wito
huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Dkt. Michael Francis wakati akifungua Baraza Kuu la
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), tarehe 18
Mei 2019.
Akizungumza
katika kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dar
es Salaam, Dkt. Francis alisema kuwa miongoni mwa namna za kushirikisha
wafanyakazi katika mipango na maamuzi ni kupitia Mabaraza ya Wafanyakazi Sehemu
za Kazi ambayo yapo kwa mujibu wa sheria na kwamba lengo kuu la kuanzishwa
kwake ni dhana ileile ya ushirikishwaji wa wafanyakazi.
Alisema,
Mabaraza ya Wafanyakazi Sehemu za Kazi yanatoa fursa bora ya majadiliano,
ushirikiano na ushirikishwaji katika maamuzi kwa kuwa yanaundwa na utatu
unaohusisha Menejimenti za Taasisi; Serikali, (hususani kupitia Wizara yenye
dhamana ya Kazi na Ajira); na Wafanyakazi kupitia uwakilishi wa maeneo
mbalimbai ya sehemu za kazi na vyama vyao vya wafanyakazi.
Aliongeza
kuwa waajiri pia wanatakiwa kuwa walinzi na kimbilio la wafanyakazi pamoja na
kuwapa motisha ili kuwasaidia kuongeza ufanisi katika kazi zao.
“Menejimenti
wapeni fursa wafanyakazi, muwasikilize, fungueni milango kwa wafanyakazi na
wapeni motisha. Hiyo husaidia kuwafanya wafanyakazi wapende kazi na kuongeza
bidii ambayo inaleta tija kazini,” Alisema.
Kwa
upande mwingine, Dkt. Francis aliwakumbusha wafanyakazi kutii mamlaka na
kutimiza wajibu wao kazini, kwani mishahara wanayolipwa ni kwa ajili ya kufanya
kazi na si vinginevyo.
Akitoa
shukrani kwa Mgeni Rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu aliiomba
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuikumbuka VETA na kuipa
kipaumbele inapoomba nafasi za kuajiri, kwani taasisi ni kubwa na inazidi
kupanuka, hivyo mahitaji ya wafanyakazi sasa ni makubwa.
Aliongeza
kuwa VETA inachukua muda mrefu kuandaa walimu wa kufundisha ufundi stadi na
wanapostaafu huacha pengo kubwa, kwani watu wenye ujuzi wa kufundisha ufundi
stadi kujaza nafasi zilizoachwa wazi huwa ni shida kuwapata, hivyo kuiomba
serikali kufikiria namna ya kusaidia kukabiliana na changamoto hiyo.
No comments:
Post a Comment