Chuo cha VETA Kihonda
kimetoa mafunzo kwa madereva wa magari makubwa zaidi ya 1500 kwa kipindi cha
kuanzia mwezi Januari mwaka huu lengo likiwa ni kupunguza ajali ambazo zinatokana
na makosa ya kibinadamu.
Chuo cha VETA Kihonda
ni Chuo ambacho kimebobea katika utoaji wa mafunzo ya udereva magari makubwa
ambapo madereva wa magari makubwa wanatakiwa kupata mafunzo hayo hapo au vyuo
vingine vilivyosajiliwa vikiwa na mafunzo hayo.
Mwalimu wa Udereva wa
Magari Makubwa na Mabasi wa chuo cha VETA Kihonda William Munuo amesema kuwa
madereva wengi wanajua kuendesha kwa kunyoosha katika barabara lakini kurudi
nyuma ni tatizo ambapo wengi ndio wanasababisha ajali au kuangusha magari hayo na
kuleta hasara kwa makampuni.
Munuo amesema mafunzo
waliyoyaanza ni endelevu na kutaka madereva kuzingatia mafunzo hayo na kuyaishi
katika kuendesha na hatimaye watakuwa madereva bora.
Munuo amesema mafunzo
hayo yanafanya magari makubwa kuishi muda mrefu kutokana na wakati mwingine
yanapata ubovu kwa uendeshaji usiofuata utaratibu wa uendeshaji wa magari hayo.
Amesema kuwa licha ya
kuwa na leseni madereva wa magari makubwa wanahitaji mafunzo ya mara kwa mara
kutokana na teknolojia za magari kubadilika kila mara.
Aidha amesema katika
mafunzo ya vitendo baadhi wanajua kuendesha magari makubwa ya tela moja wengine
ni wale wa tela mbili ambapo wanaweza wote kuendesha lakini wakiwekwa katika
urudishaji gari hizo nyuma kuna changamoto hivyo changamoto hizo zinatatuliwa
kwa kuwapa mafunzo.
"Hatuwezi
kuwaacha watu waendelee kuendesha magari makubwa katika ujuzi wa mazoea lazima
wapate mafunzo bora ya kuweza kuwa madereva bora na sio bora
madereva"amesema Munuo.
Munuo ameyataka makampuni
kuhakikisha madereva wao wanapata mafunzo kila mara kwa faida ya kampuni hizo
na kusaidia utunzaji wa magari hayo.
No comments:
Post a Comment