Mamlaka
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeibuka Mshindi wa Kwanza katika
kundi la Elimu, Utafiti na Uendelezaji Ujuzi na Mshindi wa Tatu wa Jumla katika
maonesho ya 43 ya Biashara Kimataifa Dar es Salaam (Sabasaba) yanayofanyika
viwanja vya Mwalimu J.K Nyerere jijini Dar es Salaam.
Maonesho
hayo yalifunguliwa rasmi Jumanne, tarehe 2 Julai 2019 na Mhe. Samia Suluhu
Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia alitunuku
vikombe kwa washindi wa kwanza wa makundi mbalimbali na washindi wote wa jumla.
Katika
kundi la Elimu, Utafiti na Uendelezaji Ujuzi VETA ilifuatiwa na Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam kilichoshika nafasi ya pili na Taasisi ya Uhasibu (TIA) iliyoshika
nafasi ya tatu.
Maonesho
hayo yameshirikisha makampuni, taasisi na mashirika ya ndani 3,250 ambapo washindi
wa jumla walikuwa ni Jeshi la Magereza lililoshika nafasi ya Kwanza, Jeshi la
Kujenga Taifa nafasi ya pili na VETA nafasi ya Tatu.
Akizungumza
baada ya kukabidhiwa tuzo za ushindi huo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka wa VETA
Dkt. Pancras Bujulu amesema kuwa tuzo hizo zinatoa hamasa ya kufanya kazi kwa
kujituma pamoja na kuendelea kubuni vitu mbalimbali kwa ajili ya kutatua
changamoto mbalimbali katika jamii.
Amesema
VETA pia inatekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa vyuo ili kuwafikia
watanzania wengi katika utoaji mafunzo na uendelezaji ujuzi kwa maendeleo ya
viwanda na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Maonesho
ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (Sabasaba) yalianza tarehe 28 Juni 2019 na yanatarajiwa
kuhitimishwa tarehe 13 Julai 2019 na yana Kauli mbiu ya “Usindikaji wa Mazao ya
Kilimo kwa Maendeleo Endelevu ya Viwanda.” Nchi 35 zinashiriki katika maonesho
hayo.
No comments:
Post a Comment