Serikali kupitia
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetenga Sh. bilioni 40 kwa ajili ya
ujenzi wa vyuo 25 vya Ufundi Stadi katika Wilaya mbalimbali nchini.
Akizungumza katika
hafla ya uzinduzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Urambo tarehe 9 Julai
2019, Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema ujenzi
wa vyuo hivyo ni utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuhakikisha vijana wengi
zaidi wanapata fursa za mafunzo ya Ufundi Stadi.
Prof. Ndalichako amesema
vyuo hivyo vinatarajiwa kujengwa katika Wilaya za Chunya, Kilindi, Korogwe, Ukerewe,
Igunga, Pangani, Kishapu, Rufiji, Uyui, Kwimba, Bahi, Mafia, Longido, Mkinga, Uvinza, Ikungi, Iringa
vijijini, Lushoto, Mbarali, Monduli, Buhigwe, Ulanga, Masasi, Butiama na
Chemba.
Amesema kuwa lengo la
Serikali ni kuhakikisha inakuwa na chuo cha Ufundi Stadi katika kila Wilaya na
Mkoa ili kuendana na kasi na maono ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga
uchumi wa viwanda.
“Hatuwezi kuzungumzia
uchumi wa viwanda bila kuwa na watu wenye ujuzi ambao ndio wataenda kufanya
kazi katika viwanda ndiyo maana Wizara yangu imeongeza kasi ya ujenzi wa vyuo
vya VETA nchini,” Alisema
Waziri Ndalichako amesema
kuwa kwa sasa Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa vyuo vya Wilaya za
Nkasi, Ileje, Newala, Muleba, Kasulu, Itilima, Ngorongoro, Chato na Babati vinavyotarajiwa
kumalizika ndani ya mwaka 2019 na matayarisho yanaendelea ya kuanza ujenzi wa
vyuo vya Ufundi stadi katika Wilaya za Kongwa, Ruangwa, Nyasa na Halmashauri ya
mji wa Kasulu.
Kwa ngazi ya Mkoa,
Prof. Ndalichako amesema kuwa ujenzi wa vyuo vya Mikoa ya Geita na Rukwa unaendelea
na kwamba ujenzi wa vyuo vya Mikoa ya Simiyu, Ludewa na Kagera utaanza punde.
Alisema kuwa serikali inaamini kuwa chuo hicho
cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Urambo kitakuwa chachu ya maendeleo ya viwanda Mkoani
Tabora na kuwataka wananchi wakitumie vyema katika kujipatia ujuzi.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora
Aggrey Mwanri alisema kuwa chuo cha VETA Urambo kimekuja wakati mwafaka ambapo changamoto
ya ukosefu wa ujuzi ni kubwa hali inayosababisha vijana kukosa ajira kwenye
miradi mbalimbali mkoani hapo.
Aliwasisitiza
wananchi wa Urambo kutumia vyema chuo hicho kupata ujuzi wa aina mbalimbali kwa
kuzingatia mahitaji halisi ya soko la ajira ili waweze kujiajiri.
“Tufike mahali vijana
wetu wa mkoa wa Tabora wakiulizwa unataka kuwa nani waseme wanataka kuwa
waajiri wa watu wengine”Alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya
Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi, Peter Maduki alisema kuwa VETA imedhamiria kuongeza udahili wa mafunzo
ya Ufundi stadi nchi nzima, kuboresha ufundishaji kwa kuongeza vifaa na walimu
pamoja na kuboresha miundombinu.
Alisema kuwa VETA
imejipanga kukuza uzalishaji katika viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kwa
kufanya ubunifu utakaowezesha kuanzishwa kwa viwanda pamoja na kurahisisha
uchakataji wa mazao mbalimbali.
Awali Mkurugenzi Mkuu
wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema kuwa chuo cha Urambo kilitokana na kukarabatiwa kwa majengo
yaliyotumiwa na mkandarasi aliyejenga barabara ya Ndono hadi Urambo na kisha
kukabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya
Urambo na baadae Halmashauri hiyo kuyatoa yatumike kunzisha chuo hicho kutokana
na uhitaji mkubwa wa Chuo cha Ufundi Stadi katika Wilaya hiyo.
Alisema jumla ya kiasi cha Sh. milioni 218 zimetumika
kwa ajili ya ukarabati wa chuo hicho chenye majengo 15 yatakayotumika kwa ajili
ya madarasa, karakana, ofisi, mabweni na nyumba za walimu.
Dkt Bujulu alizitaja fani zitakazotolewa katika
chuo hicho kwa kuanzia kuwa ni Umeme wa
Majumbani, Ushonaji, Ujenzi, na Uhazili na matumizi ya Kompyuta na kina uwezo
wa kudahili wanafunzi 160 kwa mafunzo ya muda mrefu na wanafunzi zaidi ya wanafunzi
500 wa kozi za muda mfupi kwa mwaka.
Aliiomba Halmashauri ya Wilaya ya Urambo
kuwaongezea eneo zaidi linalopakana na chuo hicho kwa ajili ya kuongeza
madarasa, karakana na mabweni ili kuongeza udahili wa wanafunzi kwa kuongeza
fani mbalimbali kama vile fani za kilimo na ufugaji, Uungaji na Uundaji vyuma,
ufundi mekanika, ufundi bomba, n.k. kwa kadri ya mahitaji ya soko.
Naye Mbunge wa Urambo Mashariki Magareth Sitta
aliipongeza VETA kwa kufanikisha ukarabati wa chuo hicho na kuwataka wazazi
kuwapeleka watoto katika chuo hicho wajipatie ujuzi.
Ili kuleta hamasa kwa wazazi kuleta watoto wao
katika chuo hicho, Mbunge huyo aliahidi kuwalipia ada ya kiasi cha Sh. 60,000 kwa
kila mwanafunzi kwa wanafunzi 62 kutoka katika viijiji mbalimbali Wilayani
hapo.
No comments:
Post a Comment