Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe ameushauri
uongozi wa Mamaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kufikiria wazo la
kujenga chuo kingine cha Walimu wa Ufundi Stadi ili kukidhi mahitaji ya walimu
hao ambayo yanaonekana kuongezeka kwa kasi.
Prof.
Mdoe ameyasema hayo leo, Jumatatu tarehe 9 Septemba 2019 alipofanya ziara VETA
Makao Makuu na kwenye vyuo vya VETA Dar
es Salaam na Kipawa kwa lengo la kujifunza
zaidi juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka.
Licha
ya kupongeza juhudi zinazofanywa na VETA kupanua fursa za elimu na mafunzo ya
ufundi stadi kwa kujenga vyuo vipya katika maeneo mbalimbali, amesema juhudi
hizo zinaonesha kuzaa hitaji kubwa la walimu wa kufundisha ufundi stadi, hivyo
kutegemea chuo kimoja pekee cha Walimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC)
hakutaweza kukidhi mahitaji ya walimu hao.
“Fikirieni
ama kukipanua zaidi chuo hicho au wazo la kujenga kingine pengine Dodoma, vinginevyo
mnaweza kuwa na vyuo vingi lakini mkakosa walimu wa kuvihudumia,” Alisema.
Ameongeza
kuwa ili kuhakikisha ubora wa mafunzo unazingatiwa, suala la kuwa na walimu
wenye elimu stahiki wa kutosha kufundisha vyuo mbalimbali vinavyoendelea
kujengwa ni la kuzingatia.
Sambamba
na hilo, akiwa katika Chuo cha TEHAMA cha VETA Kipawa, alifurahishwa kushuhudia
mafunzo ya Ufundi wa Simu za Mkononi yaliyoanza kutolewa chuoni hapo hivi
karibuni kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kuwataka
wanafunzi wa darasa la awali kufanya juhudi ili hatimaye baada ya kufuzu
wakaendeshe shughuli zao wakiwa na ujuzi
rasmi na wenye kuaminika.
“Nimefurahi
kuona urasimishaji wa ufundi wa simu za mkononi, bila shaka ninyi mtakuwa
mafundi bora na hamtaharibu simu za watu,” alisema.
Naibu
Katibu Mkuu huyo alipata pia fursa ya kutembelea karakana za Chuo cha Ufundi
Stadi na Huduma cha Dar es Salaam (VETA Dar es Salaam-Chang’ombe) ambapo
alishuhudia mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa chuo hicho na kuzungumza nao.
No comments:
Post a Comment