Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichao (Mb), leo tarehe 30 Septemba,
2019 amezindua rasmi kiwanda cha kisasa cha kutengeneza samani cha VETA,
kilichopo katika Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma Dodoma (VETA Dodoma RVTSC).
Kiwanda hicho
kimegharimu shilingi 3,378,086,721 hadi kukamilika. Gharama hiyo inajumlisha
gharama za Mshauri Elekezi, Mkandarasi wa Ujenzi, na Ununuzi wa Mashine na
mitambo ya kiwanda hicho. Kiwanda kimeshaanza uzalishaji na kinatoa samani za
kiwango cha juu cha ubora kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya kiofisi na
majumbani. Hivyo kitapunguza utegemezi wa samani kutoka nje ya nchi pamoja na
kusaidia wanafunzi wa fani ya useremala kufanya mazoezi ya vitendo kwenye
mashine za kisasa.
Akizungumza kabla ya
kumkaribisha Waziri, Mweyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi, Bw. Peter Maduki alisema VETA itatumia kiwanda hicho pia kuendeleza
ubunifu katike eneo la useremala, kwani kina mashine za kisasa zinazoweza
kufanya mambo mbalimbali katika shughuli za useremala.
Vilevile, alisema
kuwa kiwanda hicho ni fursa kwa mafundi seremala na wafanyabiashara wa samani
katika jiji la Dodoma, kwani wanaweza kutumia mashine za kiwanda hicho kuchonga
na kukereza mbao zao kwa ajili ya utengenezaji wa samani bora za aina na miundo
mbalimbali.
Akiwahutubia wananchi
katika uzinduzi wa kiwanda hicho ambao uliambatana na sherehe ya mahafali ya 36
ya Chuo cha VETA Dodoma, Mhe. Prof. Ndalichako, licha ya kuipongeza VETA kwa
ujenzi wa kiwanda bora na cha kisasa, aliziomba taasisi za serikali na wananchi
kwa ujumla kukitumia kiwanda hicho kujipatia samani bora na kwa bei nafuu.
Aliwahimiza watendaji
wa VETA kuhakikisha kiwanda hicho kinajiendesha kibiashara ili kuleta faida na
ikiwezekana kirudishe gharama iliyotumika kukijenga ili itumike kujenga viwanda
vingine.
Akitoa maelezo
mafupi, Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema kuwa mradi wa
ujenzi wa Karakana ya Kisasa ya Utengenezaji Samani ni miongoni mwa miradi
mbalimbali inayotekelezwa na VETA katika vyuo mbalimbali hapa nchini, kwa lengo
la kuboresha mafunzo ya ufundi stadi yanayoendeshwa katika mfumo wa vitendo, ili
kutoa wahitimu mahiri wanaohitajika katika soko la ajira na wanaoweza kujiajiri
na kuajiri vijana wenzao.
Aliitaja miradi
mingine kuwa ni kiwanda cha nyama cha VETA Dodoma; hoteli za VETA za Dodoma,
Njiro (VHTTI) Arusha, Mikumi, Tanga na Mtwara, pamoja na miradi ya ujenzi na
uboreshaji wa karakana na ununuzi wa vifaa katika vyuo mbalimbali vikiwemo
Kihonda, Manyara, Arusha (Oljoro), Lindi, Kibaha, Mbeya na Mwanza.
Naye Kaimu Mkurugenzi
wa VETA Kanda ya Kati ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha VETA Dodoma, Bw. Ramadhani
Mataka, akitoa historia kuhusu kiwanda, alizitaja faida zinazotarajiwa katika
mradi huo kuwa ni kutengeneza samani bora kwa matumizi ya serikali, mashirika
mbalimbali na watu binafsi; kutoa mafunzo ya utengenezaji wa samani zilizo bora
kwa wanachuo wa VETA ili kuendana na njia za kisasa za uzalishaji malighafi
viwandani; kutoa mafunzo kwa wahitimi wa VETA (incubation) na kuongeza mapato
kwa serikali.
No comments:
Post a Comment